Wahubiri wanavyokoroga dini nchini
VALENTINE OBARA na AGEWA MAGUT
SIFA ya kanisa iliendelea kuharibika Jumatatu, baada ya wahubiri wawili maarufu kuendelea kuanikwa kwa madai ya uhalifu.
Hii ni baada ya wahubiri James Ng’ang’a wa Neno Evangelism Ministry na David Kariuki Ngari (Gakuyo) wa Calvary Chosen Centre, kukabiliwa na madai ya kutishia maisha na kuwalaghai raia mamilioni ya pesa mtawalia.
Haya yametokea huku mienendo ya viongozi wengi wa kidini nchini ikiwa ni kinyume na mahubiri ya Biblia.
Bw Ng’ang’a alikamatwa Jumapili usiku na kufikishwa katika makao makuu ya Mkurugenzi wa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) kwenye barabara ya Kiambu ili kuhojiwa kuhusu madai ya kumtishia maisha mwanahabari wa Citizen TV, Linus Kaikai.
Hii ni baada ya kanda ya video kuonyesha mhubiri huyo akimtishia maisha Bw Kaikai wiki jana, baada ya mwanahabari huyo kuwakemea wahubiri waongo wanaolaghai wafuasi wao.
“Wewe kijana wachana na mambo zako… na kama umeingia laini ya Pastor Ng’ang’a, rafiki yangu utakipata…wewe utakimbia tu,” akasema Ng’ang’a kwenye video hiyo.
Ng’ang’a pia anakabiliwa na kesi ya kumuua mwanamke kwa kuendesha gari kwa njia hatari.
Bw Kaikai alikuwa amewashtumu wahubiri hao kwa kujifanya wanamwabudu Mungu, ilhali lengo lao kuu ni kuwatapeli waumini.
“Tunahubiriwa na wezi na siyo watumishi wa Mungu. Hawa ni walaghai wanaoishi kwa jasho la waumini wao na wanafaa kukabiliwa na polisi na mahakama,” akasema Bw Kaikai kwenye kipindi katika runinga hiyo.
Naye Kariuki aliendelea kukaangwa pale mamia ya wanaume kwa wake, vijana kwa wazee waliowekeza fedha zao kwenye kampuni yake ya ununuzi wa nyumba ya Gakuyo na Ekeza Sacco walipokita kambi alfajiri katika makao ya DCI kuandikisha taarifa, wakilenga kurudishiwa fedha zao.
Kariuki anachunguzwa kwa kuiba zaidi ya Sh1bilioni za wawekezaji wapatao 78,000. Inadaiwa alianzisha kampuni akiwa na mkewe Hannah Wachu, na kuwashauri raia kuwekeza fedha zao ili kuwasadia kuendesha biashara zao au kununua nyumba.
Ruth Wairimu, mmoja wa waliotapeliwa, alionyesha hasira zake wazi wazi jana baada ya kupoteza akiba yake yote ya Sh670,000 na Sh55,000 karo za wanawe tangu ajiunge na Ekeza Sacco miaka minne iliyopita.
Bi Wairimu aligundua ameibiwa baada ya kuomba mkopo mwaka uliopita na kuelezwa hangeweza kupata mkopo huo. Pia ombi lake la kutaka arudishiwe hela zake lilikataliwa na sasa haelewi jinsi atakavyomsomesha mwanawe, ambaye anakamilisha masomo yake ya darasa la nane mwaka huu.
Ndoto ya Stephen Njuguna ya kumiliki ardhi, nayo imezimwa baada ya kugundua alinunua ardhi hewa.
“Kampuni iliandaa safari ya kwenda Nyahururu ili tukague na kutazama ‘vipande’ vyetu vya ardhi. Hata hivyo njiani, gari lilikwama na tukaelezwa hatungefika Nyahururu kutokana na hali mbovu ya barabara. Kariuki alitwambia kwamba ardhi hiyo ilikuwa kwenye mlima ambao ulionekana kwa umbali. Kumbe tulikuwa tukichezewa tu!” akasema.
Awali jana asubuhi, wawekezaji hao walifunga barabara ya Kiambu na kuzua vurugu wakitaka kuandikisha taarifa, lakini polisi waliwatawanya kwa kutumia vitoa machozi.
DCI imewataka waliowekeza kwenye kampuni za mhubiri huyo waandikishe taarifa ili kusaidia kwenye uchunguzi ili kumfungulia Kariuki mashtaka.