Kenya tayari kukopa tena Sh370 bilioni kutoka Uchina
ANITA CHEPKOECH Na BENSON MATHEKA
Serikali inajiandaa kukopa zaidi ya Sh370 bilioni kutoka China za kujenga awamu ya tatu ya reli ya kisasa hadi Kisumu na Busia.
Ikiwa itapata mkopo huo, gharama ya reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Kisumu itakuwa ni Sh850 bilioni.
Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Reli la Kenya, Philip Mahinga alisema jana kuwa kando na kukopa pesa hizo, serikali inatafuta mkopo mwingine wa kuweka mitambo ya kulinda reli, abiria na vifaa kutoka Mombasa hadi Busia.
Kulingana na Bw Mahinga, reli hiyo inapitia maeneo yasiyo na watu wengi kama vile Suswa, na kuna haja ya kuhakikisha ni salama.
Akihutubia wanahabari kuhusu hali ya mradi huyo katika ubalozi wa China jijini Nairobi, balozi wa nchi hiyo hapa Kenya, Li Xuhang alisema pesa hizo zitakuwa mkopo wa kawaida.
“Sote tunajua kwamba awamu ya kwanza ya SGR iligharimu Sh327 bilioni na awamu ya pili iligharimu Sh150 bilioni. Kwa awamu ya tatu, mazungumzo bado yanaendelea kati ya serikali zote mbili. Hatujafikia kiwango kinachohitajika, kwa hivyo, siwezi kutaja kiwango chochote sasa hivi,” alisema Bw Mahinga, na kuongeza kuwa maelezo zaidi yatatolewa rasmi kituo cha Naivasha kitakapofunguliwa Mei.
Hata hivyo, tulidokezewa kwamba serikali inapanga kukopa Sh368 bilioni.
“SGR inahudumia watu 6,000 kila siku na tuna wasiwasi kuhusu shughuli na usalama wa vifaa vyetu katika safari za treni kutoka Mombasa hadi Nairobi na hadi magharibi mwa Kenya. Kuna haja ya kuzilinda dhidi ya ugaidi na hatari zote zinazoweza kutokea safarini. Tunaomba serikali ya China kutusaidia kuweka mitambo hii ya usalama,” alisema Bw Mahinga.
Haikubainika mitambo hiyo itagharimu kiasi kipi cha pesa.
Habari za mkopo huo zinajiri huku kukiwa na wasiwasi kuhusu uwezo wa Kenya kulipa madeni ya awali.
Pia kuna wasiwasi kuwa China inaweza kutwaa bandari ya Mombasa, Kenya ikishindwa kulipa deni la kujenga awamu ya kwanza ya SGR.