• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 10:55 AM
Tutapoteza Sh500 bilioni tukizidi kubomoa majengo – Balala

Tutapoteza Sh500 bilioni tukizidi kubomoa majengo – Balala

Na CHARLES WASONGA

MWENYEKITI wa Kamati ya Kuboresha Hali ya Jiji la Nairobi Najib Balala ameonya kuwa ikiwa shughuli ya ubomoaji majengo yaliyojengwa kando ya mito itaendelea uchumi wa nchi utapata hasara ya Sh500 bilioni.

Akiongea Jumatano alipofka mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Ardhi Bw Balala ambaye ni Waziri wa Utalii alisema tayari majengo 5,000 yanalengwa kubomolewa jijini Nairobi.

“Hasara ya ubomoaji wa majengo hayo ni Sh500 bilioni na itakuwa na athari kubwa kwa uchumi. Kwa hivyo, kabla ya kamati husika kuendelea inapasa kushauriana na wadau wote ili kupata mwafaka kuhusu ulipaji ridhaa na masuala mengineyo,” akasema Bw Balala.

Waziri huyo pia alitaka jopo hilo linalojumuisha maafisa wa kaunti ya Nairobi, Mamlaka ya Mazingira (NEMA) na asasi nyinginezo kushauria na vyama vya wakazi kabla ya kuendelea na zoezi hilo.

Kamati hiyo ya Seneti inayoongozwa na Seneta wa Nyandarua Mwangi Githiomi ilitaka jopo linaloongoza ubomoaji huo kutenda haki kwa Wakenya ambao wamewekeza rasilimali zao katika majengo hayo yaliyoidhinishwa na asasi mbalimbali za serikali.

“Sio haki kwamba wale wanapata hasara ni Wakenya wa kawaida ambao walipewa idhini ya kujenga majengo hayo ilhali maafisa wa serikali waliowapa vyeti hivyo wanasazwa,” akasema Bw Githiomi.

“Tunataka kuona haki ikitendewa wahusika wote, wajenzi na maafisa wa serikali, kwa usawa.

Akijibu Bw Balala aliwahakikishia wanachama wa Kamati hiyo kwamba Rais Uhuru Kenyatta na maafisa wakuu wa serikali wamejitolea kuhakikisha kuwa maafisa walioidhinisha ujenzi wa majengo hayo wanachukuliwa hatua za kisheria.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Seneta wa Nyandarua Mwangi Githiomi (kati) na wenzake wakiwahojia Balala na maafisa alioandamana nao. Hapa ni ndani ya majengo ya bunge Nairobi. Picha zote: Charles Wasonga.

“Bw Mwenyekiti na wanachama, ningependa kuwahakikishia kuwa tunachukulia suala hili kwa uzito sawa na ninyi. Rais Kenyatta pia anachukulia suala hili kwa uzito na ameonyesha kujitolea kwake kuhakikisha kuwa maafisa ambao kwa njia moja ama nyingi waliruhusu ujenzi wa majengo kando ya mito wanachukuliwa hatua za kisheria, ” akasema Bw Balala.

Katibu wa Wizara anayesimamia Idara ya Nyumba Hinga Mwaura kwa upande wake alisema hakuna majumba ambayo yatabomolewa kabla ya uchunguzi wa kina kufanya, ripoti kuandaliwa na kuidhinishwa na wataalamu kutoka Serikali ya Kitaifa na ile ya Kaunti ya Nairobi.

Shughuli ya ubomoaji wa majengo yaliyojengwa kando ya mito na maeneo chepechepe ilianza Agosti mwaka jana kupitia ubomoaji wa jumba la Southend, jumba la kibiashara katika eneo la Langata na jumba la kibiashara la Taj Mall.

Majengo mengine yaliyobomolewa na Mkahawa wa Java na Kituo cha Petroli cha Shell katika mtaa wa Kileleshwa, jumba la Ukay Centre na Gand Manor Hotel lililoko katika eneo la Gigiri.

Ni kufuatia ubomoaji huu ambapo Seneta wa Nairobi aliwasilisha malalamishi katika seneti, kwa niaba ya waathiriwa, kutaka maelezo kuhsu sera iliyoongoza shughuli hiyo na iwapo waliopoteza mali watalipwa ridhaa.

Wiki ijayo kamati hiyo itakutana na Gavana wa Nairobi kupata maelezo zaidi kuhusui suala hilo.

You can share this post!

Mpango wa KFS kuzindua huduma za feri Ziwa Turkana

Mvutano bungeni Keter akikataa kujibu maswali kuhusu mradi...

adminleo