Kimataifa

Mlipuko katika kiwanda cha kemikali China wasababisha vifo vya watu 44

March 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHARIKI

WATU 44 wameuawa huku wengine 600 wakijeruhiwa katika mlipuko uliotokea katika kiwanda kimoja cha kutengeneza kemikali ya kuangamiza wadudu mashariki mwa China, shirika la kitaifa la habari lilisema Ijumaa.

Mlipuko huo, ambao ulisababisha mtetemeko mdogo wa ardhi katika jimbo la Jiangsu, ndio wa hivi punde kusababisha maafa katika msururu wa ajali viwandani nchini humo ambazo zimewakera wananchi.

Mlipuko huo ulitokea Alhamisi usiku katika eneo la viwandani la Chenjiagang Industrial Park, jijini Yancheng.

“Hatimaye moto ulioandamana na mlipuko huo uliweza kudhibitiwa jana saa kumi alfajiri,” runinga ya kitaifa ikaripoti.

Watoto wa shule moja ya chekechea karibu na eneo hilo pia walijeruhiwa katika mlipuko huo.

Majeruhi walikimbizwa katika hospitali 16, 640 miongoni mwao wakitibiwa kwa majeraha madogo ya moto. Wengine 32 walipata majeraha mabaya zaidi na kulazwa katika hospitali hizo.

Zaidi ya wahudumu 3,500 wa afya waliletwa kuwahudumia waathiriwa wa mkasa huo.

Rais Xi Jinping ambaye yuko nchini Italia kwa ziara ya kikazi, aliamuru mashirika yote ya kutoa misaada yawasaidie waathiriwa ili “kudumisha uthabiti wa kijamii”.

Sharti asasi za serikali zichukue hatua zifaazo kuzuia kutokea kwa ajali kama hizo na wabaini chanzo cha mlipuko huo haraka iwezekanavyo, Xi akaongeza.

“Katika siku za hivi karibuni kumekwua na msururu wa ajali aina hiyo. Idara husika zinapasa kupata funzo ili kuzuia visa kama hivi,” taarifa hiyo ilimnukuu Rais Xi akisema.

Moto waenea

Moto huo uliotokea katika kampuni inayomilikiwa na Kampuni ya Tianjiayi Chemical, ulienea katika viwanda vingine vya karibu.

Takriban wakazi 1,000 katika eneo hilo jana walihamisha hadi maeneo salama kuwakinga dhidi ya athari za mlipuko huo, ukasema utawala wa jiji hili katika taarifa iliyotumwa katika ukurasa wake kwenye mitandao ya kijamii.

Uchunguzi unaendeshwa kubaini chanzo cha mkasa huo, lakini kampuni husika ambayo huzalisha aina 30 za kemikali, nyingine ikiwa rahisi kushika moto, imewahi kushtakiwa na kutozwa faini kwa kukiuka kanini za usalama mahala pa kazi, gazeti la China Daily lilisema.

Utawala wa mkoa wa Jiangsu umeazisha ukaguzi wa viwanda vinavyozalisha kimekali kulingana na ilani iliyochapisha katika vyombo vya habari Ijumaa.

Taarifa hiyo ilisema kuwa serikali itafunga kiwanda chochote cha kemikali ambacho kitapatikana na hatia na kukiuka sheria na kanuni kuhusu kemikali hatari.

Msururu wa ajali ambazo zimekuwa zikitokea nchini China viwandani na katika matimbo ya madini umewakera raia wa nchini. Inasemekana kuwa visa hivyo vimetia doa katika ukuaji wa kiuchumi uliodumu kwa miongo mitatu nchini humo.