MakalaSiasa

JAMVI: Wandani wa Ruto wamtaka amkabili Uhuru akigombea kiti cha Waziri Mkuu 2022

March 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na PETER MBURU

MJADALA kuhusu kuandaliwa kwa kura ya maamuzi baada ya timu BBI iliyoundwa na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga walipoafikiana mnamo Machi 9, 2018 kukamilisha kazi yake, unazidi kushika kasi.

Miezi kadhaa iliyopita, Rais Kenyatta na Bw Odinga walidokeza kuwa refarenda itaandaliwa kufanyia marekebisho katiba, ili viti fulani viongezwe serikalini.

Akizungumza alipokuwa eneo la Nyanza Desemba mwaka jana, Rais alisema kuwa hakuna haja ya kiongozi mmoja kuwa na mamlaka yote, kisha hali hiyo isababishe mizozo. “Ikiwa hiyo ndiyo sababu inawafanya watu fulani kuhisi wametengwa na serikali, sharti tujiulize ‘ni kitu kizuri au la’,” Rais alisema.

Aidha, Bw Odinga mwaka huu alidokeza kutafanyika mabadiliko ya uongozi. “Tunataka kuangalia muundo wa uongozi na kuona panapohitaji kurekebishwa. Tunataka kubadilisha nchi hii na shughuli za mabadiliko zinaendelea. Yeyote asiyetaka kusonga na mabadiliko ataachwa nyuma.”

Hii ilikuwa licha ya kuwa Naibu Rais William Ruto amekuwa na pingamizi kuhusu kubadilishwa kwa katiba kwa ajili ya kuongeza viti fulani serikalini.

Dkt Ruto amekuwa akitaja hali hiyo kuwa ubinafsi miongoni mwa baadhi ya viongozi. “Ati tuanze mjadala wa kubadilisha katiba ndio wangwana wengine wawili, watatu wapate kazi ingine, sasa tukiwa tunapangia watu wawili, watatu wapate kazi na mamilioni ya wananchi watapata kazi siku gani,” akasema.

Baada ya viongozi hao wakuu kuanzisha mjadala kuhusu uwezekano huo, waliandaa uwanja kwa viongozi wa ngazi za chini kujadili suala la kura ya maamuzi, mjadala ambao umekuwa vinywani kwa muda sasa.

Japo Naibu Rais Dkt William Ruto alikuwa akipinga mwanzoni, mambo yamekuwa yakibadilika na kambi yake ndiyo imekuwa ikiuchangamkia sana.

Hata hivyo, tangu Dkt Ruto kusema kuwa ni sawa kwa wale wanaopanga kura hiyo ya maamuzi kuendelea na maandalizi kisha wakati utakapofika yeye na wafuasi wake waamue watakapoelekea, wafuasi wake wamekuwa wakibadili wimbo.

Baadhi ya viongozi hao wamedai kuwa Rais Kenyatta hataki kwenda nyumbani baada ya kustaafu na kuwa badala yake ndiye anataka kiti hicho cha Uwaziri Mkuu, ndiposa mjadala unasukumwa.

Kuna madai kuwa serikali inayopendekezwa itakuwa na Waziri Mkuu ambaye atakuwa kiongozi wa serikali, manaibu wake wawili, Rais (ambaye hatakuwa na mamlaka kushinda Waziri Mkuu) na Naibu Rais.

Kambi ya Dkt Ruto inahisi kusalitiwa na Rais na sasa imeanza kudokeza kuwa pia nao hawatakubali kuachiwa mifupa (kwa maana ya kiti cha Urais), ikiwa mamlaka ya serikali yatahamishwa kwa afisi ya Waziri Mkuu.

Badala yake, wabunge hao wandani wa Dkt Ruto wameapa kumrai kiongozi huyo kuamua kuacha azma ya Urais na badala yake kutafuta kiti cha Uwaziri Mkuu ikiwa katiba itarekebishwa.

“Wakifikiri watabadilisha katiba eti waunde kiti kikubwa cha Waziri Mkuu sisi tuko tayari, tutamwambia William Ruto awache kugombea kile cha Urais, tutafute cha Waziri Mkuu kama hicho ndicho kitakuwa cha kuunda serikali,” akasema Bw Barasa awali mwezi huu, alipokuwa katika hafla eneo la Bonde la Ufa.

Bw Barasa ambaye alikuwa pamoja na viongozi wengine wa Jubilee, kambi ya Dkt Ruto alisema “ukijitengenezea kiti katika katiba haimaanishi hicho kiti ni chako mtu mwingine hawezi akagombea.”

Vilevile, mbunge wa Kapseret Oscar Sudi, ambaye kwa muda sasa amekuwa akimshambulia Rais Kenyatta akiwa katika hafla hiyo alisema wako tayari kuketi chini kufanya mazungumzo ya kubadilisha katiba.

“Nataka niombe Rais wetu, kama mko na mpango, kama hutaki kwenda nyumbani Bw Rais, tuambie tubadilishe hii katiba, tukae chini, tuelewane. Lakini maneno ya kuzunguka huko kando na tunajua anayelengwa ni William Ruto hatufurahii,” akasema Bw Sudi.

Kiongozi huyo katika hafla nyingine baadaye alieleza kuwa wako tayari kutengana na kambi ya Rais Kenyatta, endapo tu akitangaza wazi kuwa hamhitaji Dkt Ruto tena.

“Kama uko na maneno, wacha kutumia serikali na mkono ambao hauonekani, jitokeze useme hautaki William Ruto tena, sisi tutasikia na tutajua nini kitafuata,” mbunge huyo akasema.

Muda unavyosonga, inazidi kuwa wazi kuwa ikiwa kura ya maamuzi itaandaliwa na katiba kupitishwa kuwa kuwe na viti hivyo serikalini, huenda Rais Kenyatta na naibu wake Ruto wakajipata waking’ang’ania kiti cha Uwaziri Mkuu.

Hii ni kwa kuwa kuna dhana Bw Odinga analenga kiti cha Urais, Rais Kenyatta (ambaye ndiye mwenye mamlaka makuu sana nchini) hawezi kubali kuwa chini ya mwingine, na Dkt Ruto ambaye walikuwa na ahadi na Rais Kenyatta kuwa angeachiwa uongozi wa nchi 2022 anahisi kuwa bado ndiye anafaa kuwa mmiliki wa afisi kuu zaidi serikalini.

Baadhi ya viongozi kutoka Bonde la Ufa na pia Mlima Kenya mara kwa mara wamekuwa akikiri kuwa uwepo wa Naibu Rais ndio ulimfanya Rais Kenyatta kuingia ikulu 2013 na kuchaguliwa tena 2017.

Dkt Ruto aidha ndiye alikuwa akizunguka nchini kumwakilisha Rais katika miradi mbalimbali, wakati Rais alikuwa akisafiri kwa kazi za nje ya nchi, haswa katika muhula wa kwanza.

“Unajua fisi akitaka kula mtoto wake anamsingizia kuwa ananuka mbuzi ama kondoo. Na tayari tumeona fisi ameanza kula watoto wake, juzi amekula Rashid Echesa na wanataka kula wale wengine,” alisema Bw Barasa.

Swali kubwa sasa ni Je, wakipatana debeni mnamo 2022 wote wakitafuta kiti cha Waziri Mkuu, nani atakayembwaga mwenzake?