• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:10 PM
BERYL OONDO: Mfahamu mwigizaji stadi wa filamu kutoka Kayole

BERYL OONDO: Mfahamu mwigizaji stadi wa filamu kutoka Kayole

Na JOHN KIMWERE

NI kati ya wasanii wa kike wanaoibukia katika tasnia ya uigizaji hapa Kenya. Anasema amepania kushiriki filamu za viwango vya kimataifa siku sijazo.

Anadokeza kwamba tangu akiwa mtoto alitamani kuhitimu kuwa mwanahabari hasa mtangazaji wa runinga.

Hata hivyo alijikuta katika tasnia ya uigizaji baada ya kutamatisha elimu yake katika Shule ya Upili ya St Barbanas mwaka 2012. Alijiunga na taaluma hiyo maana talanta yake katika uigizaji aliitambua akiwa mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi ya Bright Star Kayole, Nairobi.

Je, ni nani huyu? Si mwingine bali ni binti mwenye sauti nyororo Beryl Oondo. Binti huyu ni mwigizaji, meneja wa uzalishaji wa filamu pia akishirikiana na rafikiye wanamiliki brandi inayojulikana kama Son of Man International.

Demu huyu mwenye umri wa miaka 23 anasema ”Hakika nalengakutimiza ndoto yangu hasa kushiriki filamu za kimataifa pia zipate mpenyo kuonyeshwa kwenye mojawapo ya vituo vya televisheni hapa nchini.”

Mwigizaji huyu anaendelea kunoa kipaji chake katika uigizaji ambapo huzalisha filamu kwa kutimia mwongozo wa vitabu husika ‘setbooks’ ambazo huonyeshwa katika kumbi za kijamii.

Mwigizaji mwenye sauti nyororo Beryl Oondo. Picha/ John Kimwere

Kando na brandi yao kisura huyu hufanya kazi na kundi la Fanaka Arts tangu mwaka 2014. ”Mwanzo wangu nilianza uigizaji na kundi la Changamka Arts,” alisema na kuongeza kwamba anaamini atafika mbali.

Anadokeza kuwa chini ya Son of Man International walioanzisha mwaka uliyopita wamefanikiwa kutoa filamu moja kwa jina Maxwell Easter.

”Katika mpango mzima mapema mwezi ujao tutazindua filamu nyingine iitwayo ‘The lady in red’ inayoangazia masuala ya mapenzi baina ya mwanamume na warembo wawili kutoka familia tofauti fukara na tajiri,” alisema na kuongeza kuwa wanaamini itapangawisha wapenzi wa filamu.

Beryl anasema amepania kukuza talanta yake kufikia hadhi ya mwigizaji mahiri nchini Mkamzee Mwatela ambaye humvutia kutokana na jinsi alivyoigiza katika filamu ya Mali.

Kadhalika alisema ”Pia ningependa kufikia kiwango cha waigizaji wa kimataifa kama Viola Davis na Taraji Penda Henson wazawa wa Marekani. Kwa Viola Davis huvutiwa na uigizaji wake katika filamu ya ‘How to Get Away with Murder’ pia huvutiwa na filamu ya ‘Empire’ kazi yake Taraji Penda Henson.”

Ingawa hajapata mashiko katika taaluma hiyo anashauri wasanii wa kike kwamba ni vyema kuthibitishia wazazi na jamii kwa jumla kuwa uigizaji ni ajira kama zingine.

Vile vile anawahimiza wasiwe wepesi wa kushiriki mahusiano ya kupotosha mbali wazingatie wanachohitaji wanapojitosa katika tasnia ya uigizaji. Kadhalika anawaambia wanapojitosa katika uigizaji kamwe wasijikewee matamanio ya kupata umaarufu haraka maana tasnia hiyo imejaa changamoto chungu mzima.

You can share this post!

TAHARIRI: Afisa aliyedhulumu wanahabari akamatwe

Safari ya warembo wa St Marys Ndovea hadi fainali ya Chapa...

adminleo