Jumwa aambia Ruto asitishwe na 'kelele' za ODM
Na CHARLES LWANGA
MBUNGE wa Malindi, Aisha Jumwa sasa anawataka viongozi wa upinzani wapeleke Bungeni hoja ya kumbandua Naibu Rais William Ruto uongozini, kama kweli wanaamini kuwa wana uwezo wa kuipitisha.
Akionekana kukejeli mpango huo, mbunge huyo anayezozana na chama cha ODM, alisema pendekezo la Seneta wa Siaya James Orengo, halitawahi kufanikiwa.
Akizungumza katika Shule ya Msingi ya St Andrew, eneo la Kisumu Ndogo mjini Malindi, Bi Jumwa aliwataka wanasiasa wa upinzani waache kuingiza siasa katika vita dhidi ya ufisadi.
“Bw Orengo, ambaye ninamheshimu sana alisema njia ya kupambana na Bw Ruto kutokana na madai ya ufisadi ni ndefu. Alipendekeza njia ya mkato kukabiliana naye bungeni. Chama cha ODM kinadai hayo ni maoni ya mtu binafsi. Huo ni unafiki,” akasema.
Ijumaa iliyopita, Naibu Rais aliwaahidi wafuasi wake kuwa hatatoka uongozini hadi wakati muhula wake pamoja na Rais Uhuru Kenyatta utakapokamilika.
Bi Jumwa, ambaye anakabiliana na uamuzi wa chama cha ODM kumfurusha kwa madai ya utovu wa nidhamu, alimhimiza Bw Orengo aendelee na hoja yake ikiwa ana idadi ya kutosha ya wabunge bungeni.
“Mimi ninaunga mkono hoja ya Bw Orengo ya kumshtaki Bw Ruto bungeni kama njia mojawapo ya kukabiliana na ufisadi au apeleke malamishi pamoja na ushahidi katika afisi za DCI ili achukuliwe hatua za kisheria,” alisema.
Akitoa maoni yake kuhusiana na matamshi ya Rais Uhuru Kenyatta ya kuwasilishwa kwa malalamishi katika afisi za DCI kwa wote wanaonung’unika kutokana na ufisadi, Bi Jumwa alisema Katiba imeweka utaratibu wa jinsi ya kukabiliana na ufisadi kikamilifu.
“Wale wanomchafulia Bw Ruto jina kwa madai ya ufisadi kwa ajili ya siasa za 2022, wanafaa wawache kurudisha nyuma maendeleo. Badala yake wanapaswa wapige ripoti na kupeleka ushahidi katika afisi za Tume ya Kukabiliana na Ufisadi (EACC) au afisi ya Kiongozi wa Mashtaka (DPP),” akasema.
Bi Jumwa alitoa kauli hiyo siku moja baada ya kukutana na Gavana wa Mombasa, Hassan Joho aliyeandamana na Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi, walipohudhuria kipindi cha Churchill mjini Malindi.
Mbunge huyo ambaye amekuwa akidai kuwa Bw Joho ndiye aliyemletea masaibu ya kufurushwa kwake katika chama cha ODM, alionekana akicheka na kusalimiana. Hali hiyo ilizua maoni miongoni mwa wakazi kuwa huenda wamepatana na hatua ambayo italegeza juhudi za kutimuliwa chamani.
Wakati huo huo, Bi Jumwa pia alimtaka Rais Kenyatta awanyamazishe wanasiasa wote ambao wanafanyia vita dhidi ya ufisadi siasa kwa kuamuru kushikwa na kufunguliwa mashtaka kwa kuchafua “jina zuri la nchi yetu ya Kenya.”
“Wale wanaopiga kelele na kuingiza siasa katika ufisadi wanafaa kukamatwa na kushtakiwa kwa kuchafua jina na taswira ya nchi ya Kenya kwa kuifanya kuonekana ni nchi fisadi sana ulimwenguni,” alisema na kuongeza kuwa wanafaa wamuache Dkt Ruto afanye kazi yake.
Alisema wanaomchafulia Bw Ruto jina ili aonekane mfisadi na kuleta hoja ya kubanduliwa kwake uongozini wanaogopa kukabiliana naye ana kwa ana katika uchaguzi mkuu wa 2022.
“Wawachane na Naibu Rais afanye kazi yake ya kutumikia wananchi hadi mwaka wa 2022 ambapo watakabiliana naye katika uchaguzi mkuu,” aliongeza.
Vile vile, Bi Jumwa aliwaambia wapinzani wake wanaosukuma uwepo wa uchaguzi mdogo eneo bunge la Malindi , kuwa ataendelea kutumikia hadi muhula wake utakapokamilika baada ya miaka mitano.
“Nimewaambia na ninazidi kuwaambia kuwa hakuna uchaguzi Malindi,” aliwaambia wakazi waliokuwa wamehudhuria kikao cha kutatua shida ya umiliki mashamba maeneo la Kisumu Ndogo, Majengo Mapya na Maisha Mapya.