• Nairobi
  • Last Updated March 18th, 2024 8:55 PM
Kenya U-20 kujipima nguvu na TZ na Misri kabla ya kuvaana na Rwanda

Kenya U-20 kujipima nguvu na TZ na Misri kabla ya kuvaana na Rwanda

Na GEOFFREY ANENE

KENYA na Rwanda zitapigania tiketi moja ya kushiriki mechi za raundi ya pili ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika la soka ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 nchini Niger mwaka 2019.

Katika ratiba iliyotangazwa na Shirikisho la Soka la Bara Afrika (CAF) hapo Februari 25, 2018, Kenya itaalika Rwanda kati ya Machi 30 na Aprili 1 kabla ya mechi ya marudiano nchini Rwanda kati ya Aprili 20 na Aprili 22.

Mshindi kati ya Kenya na Rwanda atalimana na mabingwa Zambia katika raundi ya pili mwezi Mei mwaka 2018.

Zambia ni baadhi ya mataifa yaliyoingia raundi ya pili bila kutoa jasho baada ya kukosa mpinzani katika raundi ya kwanza.

Mataifa mengine ndani ya raundi ya pili ni Misri, Guinea, Nigeria, Senegal, Gambia, Burkina Faso, Libya, Ivory Coast, Congo, Guinea-Bissau na Sudan.

Awamu ya mwisho ya mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Afrika itaandaliwa mwezi Julai ambapo washindi watajishindia tiketi.

Kenya, ambayo iliingia kambini Februari 25, haijashiriki mashindano ya Afrika ya chipukizi kwa muda mrefu sana. Itakuwa makini kuanza kampeni yake vyema na ufahamu kwamba mashindano ya Afrika pia yatatumika kuchagua wawakilishi wa bara hili katika Kombe la Dunia mwaka 2019.

Kabla ya kukutana na Rwanda, Kenya inapanga kujipima nguvu dhidi ya Tanzania mnamo Machi 3 jijini Dar es Salaam na Misri mnamo Machi 19 mjini Mombasa.

Sehemu ya ratiba ya mechi za kufuzu ya raundi ya kwanza:

Kenya vs. Rwanda

Mauritania vs. Morocco

Guinea Bissau vs. Sierra Leone

Algeria vs. Tunisia

Liberia vs. Benin

Gabon vs. Togo

Ethiopia vs. Burundi

Botswana vs. Namibia 

You can share this post!

Vipaji vipya vya Gor vyaisaidia kuzima Kariobangi Sharks

Idara yaomba mabilioni kujenga nyumba 500,000 za bei nafuu

adminleo