Habari MsetoSiasa

Raila apuuza dai la ODM kufifia baada ya kushindwa

April 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

BRIAN OKINDA, JUSTUS OCHIENG na RUSHDIE OUDIA

KIONGOZI wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga amezungumza kwa mara ya kwanza kuhusu kushindwa kwa wagombeaji wake kwenye chaguzi ndogo za Embakasi Kusini na Ugenya, wiki iliyopita.

Bw Odinga jana alipuuzilia mbali dhana kwamba chama hicho kimefifia katika ngome zake za kisiasa akasema hawakushindwa kwa kura nyingi na katika siasa lazima kuwe na mshindi na anayeshindwa.

“Sina wasiwasi kamwe jinsi chama kilishindwa kwenye chaguzi mbili ndogo kwa sababu tangu awali, viti hivyo vimekuwa vikipata ushindani mkali na mshindi angetoka upande wowote. Sielewi kwa nini watu wanajijazia mengi kufuatia matokeo hayo,” akasema.

Alikuwa akizungumza nje ya afisi yake iliyo Capitol Hill jijini Nairobi, baada ya kukutana na viongozi wa Rift Valley walioongozwa na Katibu Mkuu wa Chama cha KANU, Bw Nick Salat.

Katika eneobunge la Embakasi Kusini, Bw Julius Mawathe wa Chama cha Wiper alishinda kwa kura 21,628 dhidi ya Irshad Sumra wa ODM aliyepata kura 7,988 pekee.

Kwingineko Ugenya Kusini, Bw David Ochieng wa Chama cha Movement for Democracy and Growth alishinda kwa kupata kura 18,730 dhidi ya kura 14,507 za Bw Chris Karani wa ODM.

Bw Salat aliandamana na Mbunge Maalumu wa ODM, Bw Wilson Sossion na aliyekuwa Mbunge wa Eldama Ravine, Bw Musa Sirma miongoni mwa wengine. Walisema wanaunga mkono kikamilifu muafaka wa Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta pamoja na vita dhidi ya ufisadi.

Naibu Rais William Ruto na wandani wake hudai kwamba masuala hayo mawili yanatumiwa kuvuruga mipango yake ya kuotea kumrithi Rais Kenyatta kimamlaka ifikapo mwaka wa 2022.

Punde baada ya matokeo ya chaguzi hizo ndogo kutangazwa, Dkt Ruto na wandani wake walijitokeza kujigamba kwa ushindi huo kwani viongozi wa ODM walipofanya kampeni zao, waliambia wapigakura chaguzi zilihusu ufuasi kati ya Bw Odinga na Dkt Ruto , ambapo walitarajia wafuasi wa Bw Odinga wapigie kura wagombeaji wa ODM.

Viongozi mbalimbali wakiwemo wa vyama tanzu vya Muungano wa NASA, walidai ODM ilishindwa kwa sababu ya kiburi chake dhidi ya vyama vidogo, ikizingatiwa Wiper ilikuwa imeomba ODM isiwe na mgombeaji Embakasi Kusini.

Lakini Katibu Mkuu wa ODM, Bw Edwin Sifuna alisisitiza chama hicho kitazidi kuwa na wagombeaji dhidi ya vyama vingine kwenye chaguzi zijazo.

“Lazima vyama vyote vijiandae kushindana na vingine. Hakuna kitu kitapeanwa bure,” akasema.

Wachanganuzi wa kisiasa walisema ilikuwa wazi ODM ilidharau wapinzani wake ikaenda debeni bila mipango maalumu ya kutafuta ushindi.

Mhadhiri wa masuala ya kisiasa katika Chuo Kikuu cha Maseno, Bw Tom Mboya, alikosoa ODM kwa kushinda wakimtaja Dkt Ruto na masuala ya siasa za kitaifa kwenye kampeni zao badala ya kuelezea wananchi kuhusu masuala yanayowahusu moja kwa moja mashinani.