• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
Wamalwa asema hali ya ukame sio mbaya nchini

Wamalwa asema hali ya ukame sio mbaya nchini

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Ugatuzi Eugene Wamalwa amepuuzilia mbali madai kuwa hali ya kiangazi nchini ni mbaya sana.

Akiongea Jumatano, Bw Wamalwa alisema kufikia sasa serikali imeanzisha mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa wananchi milioni 1.1 walioathirika wamepewa chakula cha msaada na maji huku serikali ikisaka suluhu la kudumu kwa shida hiyo ya kiangazi ambayo hushuhudiwa nchini kila mara.

Akiongea katika makao makuu ya wizara hiyo alipotoa taswira ya hali ilivyo nchini, alisema japo Wakenya wengi wameathirika hali hiyo sio mbaya kama ilivyokuwa mnamo mwaka wa 2017.

Kulingana na Bw Wamalwa, kufikia wakati huu serikali imetoa Sh1.85 bilioni kuwasaidia wananchi walioathirika katika kaunti 13, hasa zile za Kaskazini mwa Kenya.

“Hali ya kiangazi ni mbaya zaidi katika kaunti 13, huku zile zilizoathirika zaidi zikiwa Turkana, Mandera, Marsabit, Garissa, Baringo, Kilifi, Tana River, Pokot Magharibi, Isiolo, Wajir, Samburu, Kwale na Makueni,” akasema.

Alisema hayo kwenye kikao na wanahabari baada ya mkutano wa mawaziri wanaohusika katika mipango ya kushughulikia baa la njaa nchini, akiwemo Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri.

Bw Wamalwa alisema serikali imeweka mikakati kadhaa ya kupambana makali ya njaa na ukame, ikiwemo ujenzi wa miundo msingi ya kuteka maji.

Wizara ya Maji imepewa Sh680 milioni huku ile ya kilimo ikipokezwa Sh600 milioni kufadhili mipango hiyo, akasema Bw Wamalwa.

Akaongeza: “Sh602 milioni zimetumiwa kwa Wizara ya Ugatuzi kwa ununuzi wa chakula cha msaada. Kufikia sasa magunia 26,200 ya mahindi, magunia 15,420 ya mchele na magunia 17,060 yamesambazwa kwa wanachi wanaokabiliwa na njaa kufikia sasa.”

Waziri Wamalwa alielezea hofu kwamba maeneo ya mashariki mwa nchi yatapokea kiwango kidoga cha mvua kama ilivyotabiriwa na Idara ya Utabiri wa Hali ya Anga.

“Kwa hivyo, hali haitaimarika katika sehemu kama hizi baada ya msimu ujao wa mvua ya masika,” akasema Bw Wamalwa.

You can share this post!

Maseneta wapinga mpango wa kupigwa marufuku kwa mbolea ya...

Huduma Namba itatumiwa kutoa leseni za kuendesha magari...

adminleo