• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 7:55 AM
Majaji 14 motoni akiwamo David Maraga

Majaji 14 motoni akiwamo David Maraga

Na RICHARD MUNGUTI

CHUMA ki motoni kwa majaji 14 wa Mahakama ya Juu na Mahakama Kuu ambao huenda wakatimuliwa kazini kwa madai ya ufisadi na ukiukaji wa maadili ya kazi.

Wakipatikana na hatia, majaji hawa hawatakuwa na budi ila kufurushwa kazini kwa kuletea Idara ya Mahakama fedheha.

Kesi dhidi ya majaji hawa zinaendelea kusikizwa na majopo mawili ya Tume ya Kuajiri Watumishi Idara ya Mahakama (JSC). Majopo haya yanaendelea kupokea ushahidi dhidi ya majaji hao katika Mahakama ya Juu na Jengo la Kenya R, Nairobi.

Majaji walioshtakiwa katika JSC wanawajumuisha majaji watano wa Mahakama ya Juu na majaji wanane wa Mahakama Kuu.

Walioshtakiwa ni Jaji Mkuu David Maraga, Jaji Mohammed Ibrahim, Jaji Smokin Wanjala, Jaji Njoki Ndung’u na Jaji Jackton Ojwang ambaye wiki iliyopita alisimamishwa kazi na Rais Uhuru Kenyatta.

Mwingine aliyewatangulia hawa ni naibu wa Jaji Mkuu Philomena Mwilu. Kusimamishwa kazi kwa Jaji Ojwang kumeyumbisha utendakazi katika mahakama hiyo ya upeo.

 

Rais Kenyatta aliteua jopo lenye wanachama watano kuamua hatma ya Jaji Ojwang. Mwenyekiti wa jopo hilo ni Jaji Alnashir Visram wa Mahakama ya Rufaa.

Jaji Smokin Wanjala. Picha/ Richard Munguti

Mashtaka dhidi ya CJ Maraga ni kuwa ni mbaguzi, mwenye ukabila na mkaidi wa maadili ya mahakama kwa kuhudhuria mikutano ya kisiasa Kisii na Nyamira.

Pia inadaiwa Jaji Maraga alinukuu uamuzi ambao haukuwa umesomwa wa Wajir katika kesi dhidi ya Gavana wa Laikipia.

Madai dhidi ya Majaji Ibrahim, Wanjala na Ndung’u ni ufisadi na ukiukaji wa maadili ya kazi.

Watatu hawa pamoja na Jaji Ojwang wanadaiwa walipokea hongo na kuidhinisha ushindi wa Gavana wa Wajir Mohamed Abdi Mohamud.

JSC inaombwa na walalamishi zaidi ya 600 kutoka kaunti ya Wajir wawatimue majaji hao watatu kazini kwa kupotoka katika uamuzi kwamba Bw Mohamud anahitimu kuwa Gavana.

Majaji wa mahakama kuu ni Majaji D.K Njagi, Edward Muriithi, Martin Muya, Thripsisa Cherere, Lucy Waithaka na Amin Farah. Wengine ni Richard Mwongo na James Wakiaga.

Baadhi ya malalamishi ambayo JSC imepokea ni pamoja na kucheleweshwa kutolewa kwa maamuzi, mapendeleo na muinguliano wa kimaslahi.

Majaji hawa wameandikia JSC na kueleza watawaita baadhi ya majaji wenzao kuwa mashahidi wao na walalamishi waliowasilisha kesi dhidi yao kujitetea wakiwekwa vizimbani.

JSC linaloongozwa na naibu wa mwenyekiti Mercy Deche linaendeleza vikao vyake katika Jengo la Kenya-Re.

You can share this post!

Dereva kikaangoni kuhusu madaktari wa Cuba

Muite aomba korti itupe ombi la KRA kupima fatalaiza

adminleo