• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
Si lazima tumuunge Ruto mkono 2022, wasema wazee Mlima Kenya

Si lazima tumuunge Ruto mkono 2022, wasema wazee Mlima Kenya

Na JOSEPH WANGUI

KIKUNDI cha wazee wa jamii ya Wakikuyu kimejitosa katika mjadala kuhusu siasa za urithi wa urais mwaka wa 2022 na kusema kwamba hakuna hakikisho kuwa Naibu Rais William Ruto ndiye atakayekuwa chaguo la eneo hilo.

Naibu Mwenyekiti wa kikundi hicho cha Kikuyu Council of Elders (KCE), Bw David Muthoga ambaye pia ni Naibu Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi za Mafunzo ya Matibabu (KMTC) alisema kwamba makubaliano yoyote yaliyokuwepo yalikuwa kati ya Dkt Ruto na Rais Uhuru Kenyatta na kwa hivyo jamii haikuhusika.

Msimamo huo umekuja siku moja tu baada ya Mbunge wa Gatundu Kusini, Bw Moses Kuria kusema kuwa anasajili chama kipya kitakachowakilisha maslahi ya jamii za Mlima Kenya, ishara kwamba jamii hiyo inataka kuhama Jubilee.

“Inafaa Ruto aje akutane nasi atuambie kile anachoweza kufanyia jamii hii,” akasema Bw Muthoga.

Kulingana naye, wazee wa jamii wamekuwa wakikutana na viongozi wengine wanaopanga kuwania urais 2022 akiwemo Kiongozi wa Chama cha Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, mwenzake wa Amani National Congress, Bw Musalia Mudavadi na Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga na wanazidi kushauriana na wengine.

Hata hivyo, akiwa ameandamana na Bw Mwangi Kariuki ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wapiganaji wa Mau Mau, Bw Muthoka alisisitiza kwamba msimamo wao haumaanishi kuwa kuna uadui wowote kati ya jamii yake na Wakalenjin na akaongeza kwamba ikiwa Dkt Ruto atawashawishi, basi anaweza kutekeleza masilahi yao, basi watashirikiana naye.

You can share this post!

Muuza vipuri wa River Road kizimbani kwa kuiba mali ya...

Washtakiwa kujifanya ‘wamekwama’ kimapenzi

adminleo