• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 6:55 AM
Serikali sasa yadai haikunyimwa mkopo wa SGR

Serikali sasa yadai haikunyimwa mkopo wa SGR

 BENSON MATHEKA na CHARLES WASONGA

SERIKALI ya Kenya,  ilijitetea baada ya kushindwa kupata mkopo wa Sh370 bilioni kufadhili ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Naivasha hadi Kisumu ikisema haikuwa imelipa suala hilo kipaumbele.

Kabla ya Rais Kenyatta kuondoka Kenya kuelekea China pamoja na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, iliripotiwa kuwa lengo lao kuu lilikuwa ni kupata mkopo wa kujenga reli ya kisasa hadi Kisumu na Malaba.

Akiwa Nyanza wiki jana, Bw Odinga aliunga hatua ya serikali ya kukopa Sh370 bilioni akisema reli hiyo itainua uchumi wa eneo la Magharibi ya Kenya.

Ujumbe wa serikali ya Kenya ulioongozwa na Rais Uhuru Kenyatta ulilenga kupewa Sh368 bilioni kuendeleza mradi huo katika awamu yake ya 2B.

Hata hivyo, Serikali ya China ilikataa kutoa mkopo huo ikisema haijashawishika kuwa mradi huo unaleta faida.

Wengi wa waliotoa hisia zao kwenye mitandao ya kijamii walisema kuwa Kenya inapaswa kuelekeza juhudi zake katika ulipaji wa mzigo wa deni lake ambalo sasa limetimia Sh5.4 trilioni.

Hata hivyo, mnamo Ijumaa, waziri wa uchukuzi James Macharia aliyekuwa kwenye ujumbe wa Kenya alisema serikali haikupata mkopo huo kwa sababu haukuwa na masharti nafuu.

Alisema Kenya itakarabati reli ya zamani (MGR) ili kufanikisha uchukuzi kutoka Naivasha hadi Magharibi ya Kenya. Kulingana na Bw Macharia, ukarabati huo utagharimu serikali Sh40 bilioni badala ya takriban Sh400 bilioni ilizotaka kukopa.

Wakenya walifurahishwa na Kenya kunyimwa mkopo huo wakisema pesa hizo zingeporwa na kuwaongezea mzigo wa kulipa kodi.

@Diplomacy_Kenya @Trackmann aliandika kwenye Twitter: “Mungu wa masikini halali kabisaa, mlikuwa mnadhani mtaenda mkope kwa jina letu halafu muibe zote mtuachie mzigo wa kulipa ilhali hata kupata chakula imekuwa taabu tupu…. Shindwe kabisa.”

Lakini waziri wa mashauri ya kigeni Monica Juma alikanusha kwamba sababu kuu ya ziara ya Rais China ilikuwa ni kukopa pesa za kujenga reli ya kisasa kutoka Naivasha hadi Kisumu.

Bi Juma alisema upanuzi wa reli ya kisasa kutoka Naivasha haukupewa kipaumbele katika ziara ya Rais alipoenda China wiki hii.

“Uhusiano wa Kenya na China ni mpana kuliko SGR. Ukweli ni kuwa upanuzi wa SGR kutoka Naivasha haikuwa ajenda iliyopatiwa kipaumbele katika ziara ya Beijing,” aliandika kwenye Twitter.

Bi Juma alisema lengo la serikali katika ziara hiyo lilikuwa kutafuta soko, kukuza viwanda vya humu nchini na maeneo maalumu ya kiuchumi na ushirikiano na mashirika ya kibinafsi kuhusu uwekezaji.

Alishangaa vyombo vya habari vilikotoa habari za Kenya kunyimwa mkopo.

Hata hivyo, Wakenya walisema maelezo yake yalikuwa mbinu ya serikali ya kuondoa aibu.

Aliyekuwa seneta wa Mandera Billow Kerrow na seneta wa Makueni Mutula Kilonzo walitilia shaka hatua ya serikali ya kutumia Sh40 bilioni kukarabati reli ya zamani kutoka Naivasha.

“Hata Sh40 bilioni kukarabati MGR ni nyingi sana. Hata serikali ikikanusha, tumewekewa mtego wa madeni. China haitaki kutupatia madeni zaidi kwa sababu inajua hatuna uwezo wa kulipa madeni yetu, wanataka dhamana,” alisema Bw Kerrow.

Ilisemekana Kenya na China hazikuweza kuelewana jinsi ya kudhamini mkopo huo.

You can share this post!

Atwoli akemea FKE kwa kupinga ushuru wa ujenzi wa nyumba

Wabunge wamkabili Matiang’i kwa kupokonywa walinzi

adminleo