Habari MsetoSiasa

'Nabii' akubaliana na Atwoli kwamba Ruto hatakuwa debeni 2022

April 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na TITUS OMINDE

MWANAMKE aliyejitawaza kuwa “Nabii wa Mungu” amejitokeza na utabiri unaosema kuwa Naibu Rais Dkt William Ruto hatagombea urais mwaka 2022.

Utabiri huo wa Bi Morah Mirenja, 45, kutoka kijiji cha Lusweti, Kauntindogo ya Likuyani, Kakamega unaenda sambamba na kauli ya Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyikazi (Cotu), Bw Francis Atwoli.

Wiki chache zilizopita, kiongozi huyo alikabiliwa na shutuma kali kutoka kwa wanasiasa wanaomuunga mkono Dkt Ruto, waliokerwa na msimamo wake kuwa Naibu Rais hatakuwa miongoni mwa watakaowania urais.

Dkt Ruto amekuwa kwenye kampeni tangu mwaka jana, akijaribu kushawishi ngome mbalimbali zikiwemo Pwani, Gusii, Magharibi na Mlima Kenya kumpa kura ifikapo 2022.

Lakini Bi Mirenja, ambaye anasomea taaluma ya famasia, anashikilia msimamo kuwa kama ambavyo amekuwa akitabiria wakazi mambo na yanatimia, maono yake ya sasa si ya kutiliwa shaka.

Ameandika ujumbe wa kurasa 200 ambao umeorodhesha kwa kina kila tukio linalofungamana na uchaguzi wa mwaka wa 2022.

Kupitia kwa unabii huo, Bi Mirenja anadai kuwa Mungu tayari amemwekea wakfu Rais Uhuru Kenyatta kuwa ‘mfalme’ wa nchi huku kiongozi wa ODM Raila Odinga akichaguliwa kuwa rais ambapo Naibu Rais, Dkt William Ruto pamoja na Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho watachaguliwa manaibu wa rais ifikapo 2022.

“Mungu amenionyesha kuwa kampeni zinazoendelea za 2022 ni kazi bure. Tayari ameshamtawaza Rais Kenyatta kama mfalme huku Bw Raila Odinga akitawazwa kuwa rais mwenye manaibu wawili ambao ni Dkt Ruto na Gavana wa Mombasa Hassan Joho,” alisema kwenye mahojiano na Taifa Leo nyumbani kwake.

Kulingana naye, picha kamili ya viongozi ambao wataongoza Kenya mwaka wa 2022 itaonekana wakati wa maadhimisho ya sherehe ya Madaraka Dei, Juni Mosi mwaka huu. Anadai kuwa Askofu mkuu wa makanisa ya African Divine Church (ADC), John Chabuga ameteuliwa na Mungu kuwekea wakfu viongozi ambao wataongoza Kenya 2022.