• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 8:55 AM
Congo yateketea baada ya watu wengine 49 kuuawa mapiganoni

Congo yateketea baada ya watu wengine 49 kuuawa mapiganoni

Tangu mwezi Desemba 2017, jumla ya watu 100 wameuawa katika mapigano mkoani Ituri huku zaidi ya watu 200,000 wakilazimika kutoroka makwao. Picha/ Maktaba

Na AFP

BUNIA, DRC

WATU wasiopungua 49 wameuawa katika mapigano mapya ya kikabila yaliyotokea katika mkoa wa Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), afisa mmoja wa shirika la kutoa misaada alisema Ijumaa.

Mauaji haya yanatokana na msururu wa mapigano kati ya jamii za Hema na Lendu katika mkoa huo ulioko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, maafisa wa serikali waliambia shirika la habari la AFP.

“Tumehesabu miili 49 na tungali tunasaka miili mingine, akasema Alfred Ndrabu, afisa wa mipango katika shiriki la International Catholic Charity Caritas.

“Mtoto amelazwa leo asubuhi (Ijumaa asubuhi) katika Hospitali Kuu ya Drodro, akiwa na mshale ukiwa umekwama kichwani,” Buju akaongeza.

Hata hivyo, Waziri wa Masuala ya Ndani Henri Mova alisema idadi ya waliouawa ni 33.

“Gavana wa mkoa yuko njiani akielekea katika eneo la mauaji,” Mova akasema. Mapigano hayo yalitokea katika kijiji cha Maze, kilichoko umbali wa kilomita 80 kaskazini mwa mji wa Bunia, ambao ndio mji mkuu wa mkoa wa Ituri.

Walioshuhudia kisa hicho waliambia AFP kwamba washambuliaji ni watu kutoka kabila la Lendu.

“Washambuliaji walivamia kijiji hicho na ndipo wakatekeleza unyama huo,” mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu eneo hilo Banza Charite akasema.

 

200,000 watoroka

Tangu mwezi Desemba 2017, jumla ya watu 100 wameuawa katika mapigano mkoani Ituri huku zaidi ya watu 200,000 wakilazimika kutoroka makwao.

Watu 28,000 kati yao wamekuwa wakivuka mpaka na kuingia nchini Uganda katika siku za hivi karibuni, kulingana na takwimu zilizotolewa na Umoja wa Mataifa (UN). Wengi wao wamekuwa ni watoto na wanawake.

Watu wa kabila la Hema, ambao ni wafugaji, na wale wa Lendu ambao ni wakulima, wamekuwa wakipigana kila mara tangu miaka ya 1990.

Lakini katika siku za hivi karibuni, mapigano kati yao yamezidi kutokana na uchochezi kutoka Rwanda na Uganda ambazo zimekuwa ziking’ang’ania utajiri wa dhahabu, almasi na rasilimali nyingine za misitu.

Inadaiwa kuwa mapigano yaliyotokea katika mkoa wa Ituri mwaka huu, pia yalitokana na taharuki ya kisiasa ambayo imegubika taifa hilo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Katika kipindi hicho, Rais Joseph Kabila amekuwa akijizatiti kujidumisha mamlakani licha ya muhula wake wa pili uongozini kukamilika.

Makundi ya wapiganaji yamekuwa yakiendeleza vita katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, ambayo inapakana na mataifa ya Uganda, Rwanda, Burundi na Tanzania.

 

You can share this post!

JAMVI: Uhuru apewa onyo kuhusu uasi wa kisiasa akizidi...

Mwanafunzi awaua wazazi wake chuoni na kutoroka

adminleo