• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Hofu magenge hatari ya vijana kufufuka eneo la Kisauni, Mombasa

Hofu magenge hatari ya vijana kufufuka eneo la Kisauni, Mombasa

Na MOHAMED AHMED

MAGENGE ya kutisha ya vijana wadogo wanaotumia visu kuhangaisha wakazi yamerejea mjini Mombasa.

Magenge hayo ya matineja yalikuwa yamekomeshwa mwaka 2017 kupitia operesheni kali ya polisi iliyowaangamiza wengi wao.

Hata hivyo, yamerejea tena na yanazua vurugu katika kaunti ndogo ya Kisauni ambayo imekumbwa na visa vya uhalifu.

Polisi katika kaunti hiyo wamelazimika kuanza tena operesheni ya kukabiliana na magenge hayo ambayo wanachama wake ni vijana wa miaka kati ya 12 na 24. Wanatekeleza uhalifu baada ya kutumia dawa za kulevya.

Katika miezi miwili iliyopita, magenge hayo mawili ya ‘Wakali Kwanza’, ‘Wakali Wao’ na ‘Piyo Piyo’ yamerejelea vitendo vyao vya uhalifu na kuwahangaisha wakazi wa Kisauni na Nyali.

Baadhi wanatumia bodaboda na vijigari vya tuktuk kuwavizia wakazi hususan katikati mwa jiji.

Kwa mujibu wa maafisa wanaohusika na mradi wa usalama wa jamii Kisauni, genge lingine kwa jina Piyo Piyo pia limeibuka.

Kila siku, wakazi wa maeneo ya Likoni na Kisauni huripoti visa kwa kudungwa visu na kujeruhiwa na wahalifu hao ambao pia hubeba mapanga.

Kwa mfano, Februari 5 genge la karibu vijana 20 waliokuwa na vyuma pamoja na mapanga walivamia ibada ya mazishi Mishomoroni na kutekeleza wizi.

Vilevile, jioni hiyo waliwashambulia wakazi na wenye maduka na kujeruhi watu wasiopungua sita.

Kwa mujibu wa duru za usalama, magenge hayo yamekuwa yakitekeleza uhalifu wao katika maeneo ya Soko Mjinga, Magogoni, Mishomoroni, Majengo Mapya, Barsheba na Mtopanga.

Visa vingine pia vimeripotiwa kwenye barabara ya Moi Avenue katikati mwa jiji huku wahalifu hao wakiwalenga wakazi wanaotoka kazini usiku.

 

You can share this post!

Keter na Bowen katika mtanziko baada ya Jubilee kupanga...

Shinikizo Naibu Chansela ajiuzulu kufuatia mauaji ya...

adminleo