Gaidi hatari aliyepanga kushambulia jiji la Nairobi auawa
Na FRED MUKINDA
POLISI wamemtambua kiongozi wa kundi moja la kigaidi ambaye alipanga shambulio jijini Nairobi Februari lakini likatibuliwa.
Mbarak Abdi Huka, 27, aliuawa katika makabiliano ya risasi kati yake na polisi eneo la Merti kaunti ya Isiolo mnamo Februari 15.
Vilevile, uchunguzi umebaini kuwa gaidi huyo ana uhusiano wa karibu na mhubiri mbishi Sheikh Guyo Gorsa, anayekabiliwa na kesi za ugaidi kortini.
Polisi walibaini kuwa alama zake za vidole zinafanana na maelezo kumhusu yaliyoko katika afisi ya msajili wa watu.
Mbaraka, ambaye ni kitinda mimba katika familia ya watoto wanne, alizaliwa katika eneo la Mountain, eneo bunge la Saku, kaunti ya Marsabit
Alisomea katika Shule ya Msingi ya Sakuu kati ya miaka ya 1999 na 2006.
Kati ya miaka ya 2007 na 2010, Mbarak alikuwa mwanafunzi katika Shule ya Upili ya Marsabit ambako alifanya mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE) na kupata alama ya B-
Baadaye alifanya kazi kama mwalimu wa kibarua katika shule ya Taqwa Madrasa inayoendeshwa na Sheik Gorsa.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa akiwa shuleni humo alijulishwa kwa gaidi mmoja kwa jina Hassan Jarso Kotolla aliyempeleka Somalia kwa mafunzo.
Akiwa Somalia, Mbarak alipata mafunzo ya utengenezaji mabomu na mbinu kadha za kivita.