KimataifaSiasa

Juhudi za kumwondoa Rais Zuma mamlakani zashika kasi

February 13th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Wafuasi wa Kiongozi wa Chama tawala nchini Afrika Kusini Cyril Ramaphosa wakimtaka Rais Jacob Zuma ang’atuke. Picha/AFP

Na AFP

PRETORIA, AFRIKA KUSINI

Kwa Muhtasari:

  • Kamati kuu ya ANC ilieleza dalili za awali zilionyesha kwamba Bw Zuma hakuwa tayari kung’atuka uongozini
  • Bw Zuma, aliye na umri wa miaka 75, anakabiliwa na sakata kadhaa za ufisadi kwa miaka tisa
  • Amekuwa akikataa shinikizo za kujiuzulu tangu mwezi Desemba baada ya Bw Ramaphosa kutwaa rasmi uongozi wa chama hicho
  • Bw Ramaphosa ameshikilia kwamba ANC inakumbwa na mgogoro mkubwa ambao lazima utatuliwe mara moja

MIKAKATI ya kumwondoa mamlakani Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini ilishika kasi Jumatatu, huku viongozi wakuu wa chama cha African National Congress (ANC) wakikutana ili kukamilisha mipango hiyo.

Kamati kuu ya chama hicho, ilieleza uwezekano wa kumrai kuondoka mamlakani kwa hiari, baada ya dalili za awali kuonyesha kwamba hakuwa tayari kung’atuka uongozini.

Ripoti zilisema kwamba juhudi hizo zimekuwa zikiongozwa na kiongozi wa chama, Cyril Ramaphosa, ili kuimarisha nafasi yake ya kushinda urais, katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini humo mnamo 2019.

Mnamo Jumapili, Bw Ramaphosa alikubali kwamba juhudi hizo zimekuwa zikizua mgawanyiko mkubwa katika chama hicho, ila “hawako tayari kuangalia nyuma.”

 

Suala zito

“Naelewa kwamba suala hili ni lenye uzito mkubwa, hasa katika mustakabali wa chama. Hata hivyo, hatutaangalia nyuma. Lazima tulainishe uongozi kwa manufaa ya vizazi vyetu na raia wote wa Afrika Kusini,” akasema Bw Ramaphosa.

Bw Zuma, aliye na umri wa miaka 75, anakabiliwa na sakata kadhaa za ufisadi kwa miaka tisa ambayo amekuwa uongozini.

“Tunajua mnataka uongozi mpya. Tupeni muda. Haya yatatimia tu,” akasema Bw Ramaphosa, kwenye kongamano la kuadhimisha miaka 100 tangu kuzaliwa kwa rais wa kwanza mweusi wa taifa hilo, marehemu Nelson Mandela.

Mkutano mmoja wa kamati kuu ya chama ulifutiliwa mbali wiki iliyopita ili kutoa nafasi ya mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Bw Zuma na Bw Ramaphosa, ambaye pia ndiye makamu wa rais wa nchi hiyo.

Bw Zuma amekuwa akikataa shinikizo za kujiuzulu tangu mwezi Desemba baada ya Bw Ramaphosa kutwaa rasmi uongozi wa chama hicho.

Wadadisi wanasema kwamba, ikiwa kamati hiyo itafanikiwa kumwondoa mamlakani Bw Zuma, basi itakuwa vigumu sana kwake kukataa.

 

Ufisadi

Baadhi ya sakata zinazomwandama Bw Zuma ni madai ya kushirikiana na mfanyabiashara Ian Gupta kutoka India kwenye kandarasi moja ya ununuzi wa silaha za kijeshi.

Inadaiwa kwamba wawili hawa walipokea mamilioni ya fedha kutoka kwa kampumi ambayo ilipewa kandarasi ya kuiuzia Afrika Kusini silaha hizo.

Mbali na hayo, Bw Zuma pia anadaiwa kupokea hongo katika sakata zingine, hali ambayo ilimfanya kushtakiwa na baadhi ya wanaharakati nchini humo, kwa madai kwamba alikuwa akipanga kukwepa kujibu mashtaka hayo.

Bw Ramaphosa amekuwa akishikilia kwamba chama hicho kinakumbwa na “mgogoro mkubwa katika uongozi wake” ambao lazima utatuliwe mara moja.

“Uongozi wa sasa haufai,  lazima ufanyiwe mageuzi mara moja,” akasema Bw Ramaphosa.