HabariHabari Mseto

Kamari yageuka janga kuu nchini

February 13th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Mwanamume akishirki katika mchezo wa kubashiri mechi katika mtaa wa Nyalenda, kaunti ya Kisumu. Picha/ Tonny Omondi

Na KAZUNGU SAMUEL

Kwa Muhtasari:

  • Kmari imeathiri sana uwezo wa watoto wengi kupata matokeo bora shuleni kwa sababu ya mawazo mengi
  • Uraibu huo umechangia ongezeko la idadi ya watoto wanaoacha shule na wizi nyumbani ili wapate pesa za kulipia uchezaji
  • Baadhi ya kaunti zimetangaza vita dhidi ya wanaoendesha biashara ya kamari katika juhudi za kuwanasua watoto
  • Watu kadhaa wanaswa huku mashine nyingi zikuzuiliwa baada ya misako

WAZAZI, walimu na viongozi serikalini wameeleza hofu ya kuharibiwa kwa maisha ya baadaye ya wanafunzi wengi ambao wameingia kwenye mtego wa kucheza kamari.

Hali ni mbaya katika miji na hata vijijini ambapo mashine za kamari zimesambazwa hasa na raia kutoka China.

Kulingana na Mwenyekiti wa Chama cha Kitaifa cha Wazazi, Bw Nicholas Maiyo, michezo hiyo imeathiri sana uwezo wa watoto wengi kupata matokeo bora shuleni kwa sababu wanatumia muda wao vibaya na pia wanashindwa kufuatilia masomo darasani kutokana na mawazo mengi.

Bw Maiyo aliambia Taifa Leo kuwa chama chake kimepokea malalamiko mengi kutoka kwa wazazi kuhusu jinsi watoto wachanga wanaoshiriki kamari kubadilika na kuwa watovu wa nidhamu.

 

Wizi nyumbani

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Sekondari (KESSHA), Bw Kahi Indimuli anasema kamari imechangia ongezeko la idadi ya watoto wanaoacha shule na wizi nyumbani ili wapate pesa za kulipia uchezaji.

Visa viwili vya watoto kujiua baada ya kushindwa kwenye michezo hiyo vimeripotiwa Kilifi, mmoja wao akiwa Silas Kazungu wa miaka 9, ambaye alijinyonga baada ya kukosa kushinda korosho ambazo alikuwa akichezea kamari.

Naye mtoto wa miaka 13 katika kijiji cha Chumani kaunti hiyo ya Kilifi, alijiua babake mdogo alipokataa kumpa Sh100 ambazo alikuwa ameshinda baada ya kucheza kamari.

Kabla ya kijinyonga, kijana huyo alijaribu kupigana na babake mdogo akitaka apatiwe pesa hizo lakini akashindwa nguvu na hivyo akaamua kujitoa uhai.

 

Vita kutokomeza kamari

Baadhi ya kaunti zimetangaza vita dhidi ya wanaoendesha biashara ya kamari katika juhudi za kuwanasua wakazi hasa watoto kutokana na kasumba ya kamari. Kaunti hizo ni pamoja na Murang’a na Kisii.

Mtaalamu wa masuala ya kisiasa na kijamii, Bi Maimuna Mwidau anawalaumu wazazi ambao huwaacha watoto bila uangalizi maalum, hivyo basi kuwapa nafasi ya kujihusisha na visa kama vile kamari.

“Kama wazazi lazima tujue majukumu yetu. Inasikitisha kwamba kuna wazazi wengine ambao hawafuatilii maendeleo ya watoto wao na hapo ndipo tatizo linapotokea,” Bi Mwidau alieleza Taifa Leo.

 

Pesa za haraka

Kulingana na msomi wa Sosholojia katika Chuo Kikuu cha Pwani, Prof Halimu Shauri, umaskini na nia ya kutaka pesa za haraka pia zinashawishi Wakenya wengi wakiwemo watoto kushiriki kamari.

“Wale watoto ambao walifariki Kilifi walishawishika kucheza kamari kutokana na umaskini unaoikumba jamii kwa sasa.”

Kamanda mkuu wa polisi Pwani, Bw Larry Kieng alisema kuwa msako wa kuwanasa wanaoleta mashini hizo pamoja na wamiliki unaendelea.

“Kufikia sasa tumeweza kunasa watu kadhaa. Tuko na mashine nyingi ambazo tumezizuilia na msako utaendelea hadi tuhakikishe hakuna mashine hata moja vijijini,” akasema Bw Kieng.