• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
WASONGA: Naam vyuo vya kiufundi visibadilishwe kuwa vyuo vikuu

WASONGA: Naam vyuo vya kiufundi visibadilishwe kuwa vyuo vikuu

Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC), Profesa George Magoha. Mwandishi anakubaliana naye kwamba mageuzi yaliyoletwa na dhana kwamba shahada za digrii ndizo funguo za maisha mema, yaliinyima Kenya hazina ya wataalamu wazuri wa kiufundi. Picha/ Maktaba

Na CHARLES WASONGA

TAIFA la Kenya linahitaji kuwa na vyuo bora vya kiufundi ili liweze kuzalisha nguvu-kazi ambayo itaisaidia kufikia malengo yake ya maendeleo katika karne hii.

Ukweli ni kwamba kuna idadi ndogo zaidi ya mafundi nchini, hali inayopelekea mashirika mbalimbali kusaka wataalamu hao kutoka mataifa ya nje.

Ni aibu kwamba zaidi ya miaka 50 baada ya taifa hili kupata uhuru bado linategemea mafundi bora wa ujenzi wa majumba na barabara kutoka mataifa ya nje.

Uchunguzi umebaini kuwa mafundi wenye ujuzi wa kiwango cha juu ambao huendesha miradi ya ujenzi wa barabara zinazofadhiliwa na serikali ya China hutoka huko huko.

Waama, nafahamishwa kuwa wengi wao hata huwa ni wafungwa!

Na mafundi wachache walioko nchini wamepungukiwa kiujuzi, hali inayopelekea baadhi yao kufanya kazi chapwa.

Hali hii husababisha hasara na maafa, kupitia kuporomoka kwa majengo kutokana na utendakazi duni.

Kiini cha hali hii ni kwamba kuanzia mwaka wa 2003, serikali ilikumbatia mwenendo mbaya wa kugeuza taasisi kuu za kiufundi kuwa vyuo vikuu.

Kwa mfano Chuo Anuwai cha Kenya (Kenya Polytechnic) kilibadilishwa kuwa Chuo Kikuu cha Kiufundi Kenya na kuanza kusomesha kozi za digrii.

Chuo hiki kilipoteza sifa yake ya zamani kama chuo ambacho kilifundisha kozi za kuhitimu cheti cha diploma katika taaluma mbalimbali.

Hii ndiyo maana nakubaliana na kauli ya Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC), Profesa George Magoha kwamba mageuzi hayo, yaliyoletwa na dhana kwamba shahada za digrii ndizo funguo za maisha mema, yaliinyima Kenya hazina ya wataalamu wazuri wa kiufundi.

 

Vimebadili mkondo

Inasikitisha kuwa baada ya vyuo vya zamani ya kiufundi “kupandishwa hadhi” kuwa vyuo vikuu au vyuo vikuu vishirikishi, vilianza kubadili mkondo na kuanzisha kozi nyinginezo; kama zile za sanaa.

Hii ndiyo maana serikali sasa inalazimika kuwekeza hela nyingi kila mwaka kujenga vyuo vingine vya kiufundi vya kufundisha kozi za hadi kiwango cha diploma.

Kwa mfano, katika mwaka wa fedha wa 2017/ 2018 Waziri wa Fedha Hernry Rotich alitenga Sh2 bilioni za ujenzi wa vyuo hivyo maeneo mbali mbali nchini.

Nadhani fedha kama hizi zingetumika kwa upanuzi wa vyuo kama vile, “Kenya Polytechnic”, “Mombasa Polytechnic”, “Kisumu Polytechnic”, “Eldoret Polytechnic” badala ya kuvibadilisha kuwa vyuo vikuu.

Taifa hili linastahili kubadili sera yake kuhusu masomo ya kiufundi ili iweze kuweka msingi thabiti wa maendeleo.

You can share this post!

OBARA: Ni aibu Kenya kuendelea kutegemea mvua pekee

Mvua kubwa yasababisha maafa kote nchini

adminleo