Mau Mau wadai walificha hazina ya siri kuu Mlima Kenya, wataka kukutana na Rais Kenyatta
Na WAIKWA MAINA
WAPIGANIAJI uhuru wa Mau Mau wanataka kukutana na Rais Uhuru Kenyatta kujadili jinsi ya kuchimbua hazina wanayodai iliwekwa mafichoni katika Mlima Kenya.
Wakongwe hao wanadai hazina hiyo ni siri ya viongozi wakuu wa Mau Mau akiwemo rais wa kwanza wa Kenya, hayati Mzee Jomo Kenyatta.
Walisema Mzee Kenyatta aliunga mkono azimio kwamba hazina hiyo inaweza tu kufichuliwa katika sherehe maalum ya utakaso, lakini kwa bahati mbaya aliaga dunia kabla sherehe kutekelezwa.
“Tulikuwa na agano kwamba kutafanywa sherehe ya utakaso baada ya kupata uhuru, lakini kabla ya kuondoka msituni kujiunga na familia zetu. Kiapo kiliandikwa na kufichwa katika madhabahu ya siri Mlima Kenya.
Tulihisi utakaso ulikuwa muhimu kusafisha damu iliyomwagwa wakati wa vita hivyo vya ukombozi,” akasema kiongozi wa wapiganiaji hao Brigedia John Kiboko.
Sherehe ya utakaso
Brigedia Kiboko anadai kuwa misukosuko inayokumba taifa inatokana na maagano ambayo hayajatimizwa, na iwapo sherehe ya utakaso haitafanywa laana hiyo itaandama taifa na vizazi vijavyo.
Anahofia hazina hiyo haitawahi kupatikana iwapo wapiganiaji walio hai hawatapewa fursa ya kuifichua.
Bi Wambui Gichakuri, ambaye alikuwa kapteni wa Mau Mau na pia msaidizi wa Jenerali Mathenge Mirugi wakati wa vita hivyo, alisema tambiko za Kikuyu zilizostahili kuandaliwa kabla yao kuungana na familia hazikufanywa.
Kila mmoja alifululizwa hadi ofisi za wilaya yake na kisha kupelekwa nyumbani.
“Tunataka kujadiliana na Rais Kenyatta kuhusu hazina hiyo, kama kiongozi wa taifa na kwa sababu babake alijua kuwepo kwake. Babake aliacha maagizo kuhusu hazina,” akasema.