• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 8:55 AM
Ruto kukosa nyama choma Amerika

Ruto kukosa nyama choma Amerika

Na CHRIS WAMALWA

NAIBU Rais William Ruto Jumatatu atakosa hafla ya kula nyama choma nchini Amerika baada ya ziara yake ya kuzindua vuguvugu la Tanga Tanga katika mataifa ya kigeni kufutiliwa mbali.

Waandalizi wa ziara hiyo katika jimbo la Kansas walisema wataendelea na hafla hiyo kwa sababu maandalizi yalikuwa yamekamilika.

Hata hivyo, baadhi ya Wakenya wanaoishi Amerika (US) walisema hawakufahamishwa kuhusu ziara hiyo na kuitaja kuwa ya kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022.

Dkt Ruto alipaswa kuwasili Kansas leo kwa ziara ambayo ingemfikisha Canada lakini ikazimwa na Ikulu ikisemekana hangeondoka nchini kwa sababu Rais Uhuru Kenyatta angekuwa nje ya nchi.

Hata hivyo, wafuasi wake nchini Amerika walisema wanaendelea na mipango ya kuzindua vuguvugu la Tanga Tanga katika mataifa hayo.

Akiongea na Taifa Jumapili kwa njia ya simu kutoka jimbo la Kansas, mshirikishi mkuu wa ziara ya Ruto, Bi Genevieve Jobe, alisema wanasubiri afisi ya Naibu Rais jijini Nairobi kutangaza tarehe mpya ya ziara hiyo.

Bi Jobe alikanusha ripoti kwamba ziara hiyo ilifutiliwa mbali.

“Ziara hiyo haikufutuliwa mbali ila iliahirishwa hadi siku nyingine. Tutasubiri hadi tarehe nyingine ya ziara hiyo itakapotangazwa,” Bi Jobe akasema.Hata hivyo, alisema maandilizi ya hafla ya kula Nyama Choma itakayofanyika kesho jijini Kansas City na ambayo Dkt Ruto aliratibiwa kuhudhuria yamekamilika.

“Ndiyo, hafla hiyo bado iko na tutakutana kama Wakenya kusherehekea Siku ya Ukumbusho. Kwa sababu shughuli hii ilipangwa zamani, hatuoni kama ni sawa kuiahirisha,” aliongeza na kusema imepangwa na wafuasi sugu wa Tanga Tanga Amerika.

Hafla hiyo pia itahudhuriwa na wafuasi wa Dkt Ruto kutoka jijini Jersey, jimbo la New Jersey, kulingana na kiongozi wao Bw Stephen Keter.

Bi Jobe alisema awali Naibu Rais alikuwa ametuma ujumbe uliojumuisha mshauri wake wa kisheria na mkuu wa watumishi ambao wanatarajiwa kuhudhuria hafla ya kesho jijini Kansas.

“Hii ni kwa sababu Naibu Rais alikuwa anachukulia ziara yake kwa umuhimu mkubwa,” akasema bila kutaja majina ya wawakilishi wa Dkt Ruto katika hafla hiyo.

Naibu Rais alikuwa amepangiwa kuondoka nchini Jumamosi kwa ziara ya wiki moja katika mataifa ya Amerika na Canada katika kile kilichotajwa kama sehemu ya kampeni ya kujinadi kama mgombeaji urais bora katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Naibu Rais alitarajiwa kuwasili Amerika Jumapili, kulingana na barua iliyoandikwa na Mshauri wa Kisheria katika afisi yake Dkt Korir Sing’oei.

“Ningependa kuthibitisha kuwa Naibu Rais wa Kenya atatembelea jimbo lako (Kansas) kati ya Mei 26 hadi Mei 28, 2019 katika mpango wa kuimarisha uhusiano kati ya Amerika na Kenya na watu wa mataifa hayo,” ikasema barua hiyo iliyotumiwa utawala wa jimbo hilo.

Barua hiyo pia ilisema kuwa Dkt Ruto alitarajiwa kuimarisha sekta ya elimu na kuwahutubia Wakenya wanaoishi jimboni Kansas.Kwenye taarifa, Wakenya wanaoishi Washington walisema hawakuhusishwa kwenye maandalizi ya ziara hiyo japo Dkt Ruto alipangiwa kuhutubia Wakenya wanaoishi Amerika.

Ingawa Mkurugenzi wa Mawasiliano katika Afisi ya Naibu Rais David Mugonyi alisisitiza kuwa ziara hiyo haikupanguliwa kwa sababu iligongana na ziara ya Rais Kenyatta nje ya nchi, kiongozi wa taifa hakusafiri popote Jumamosi ilivyotarajiwa.

Vilevile, hakuhudhuria hafla ya kuapishwa kwa Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, kama ilivyopangwa hapo awali.Imeripotiwa kuwa kufutiliwa mbali kwa ziara hiyo kumesababisha misukosuko katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni ambapo mmoja wa maafisa wakuu alipewa likizo ya lazima.

You can share this post!

Mke amshtaki mume kwa ulaghai wa penzi

HUDUMA NAMBA: Usajili wakamilika wachache wakijitokeza...

adminleo