Habari Mseto

Baa la njaa: Watoto sasa wazirai shuleni

February 25th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Mwanamke na watoto wake wasubiri chakula cha msaada katika kauntindogo ya Kinango, Kaunti ya Kwale wakati wa kiangazi mwaka uliopita. Kaunti hiyo inakumbwa na janga la njaa ambalo, inahofiwa, litadumu kwa muda mrefu kama mvua haitanyesha hivi karibuni. Picha/KNA

Na KNA

Kwa ufupi:

  • Wengi wa watoto hutegemea mlo mmoja pekee kwa siku, ambao wanakula usiku tu wala hawana uwezo wa kumudu kiamsha-kinywa ama chamcha
  • Baadhi ya wanafunzi wamegeukia kula maembe huku wengine wakiminya limau na kunywa maji yake ili kupunguza makali ya njaa
  • Watoto hawa wanazidi kudhoofika siku baada ya nyingine. Visa vya upungufu wa damu mwilini vimeenea kote kwa sababu ya utapiamlo
  • Wazazi wametakiwa kuwajibika zaidi na kutimiza mahitaji ya watoto wao akisema baadhi wametelekeza majukumu yao

WALIMU katika Kaunti ya Kwale wameeleza hofu yao kuhusu jinsi janga la njaa linavyoathiri masomo kwa kiwango cha kufanya watoto kuzirai madarasani.

Walitoa wito hatua za dharura zichukuliwe kwa haraka kwani wao wenyewe hawana uwezo wa kuitatua hali hiyo.

“Njia ya pekee ya kukabiliana na hali hii ni kwa serikali kufufua mpango wa kuwapa chakula wanafunzi,” alisema Bi Flora Nzisya ambaye ni mwalimu katika shule ya msingi ya Kwale.

Kulingana naye, idadi ya watoto shuleni pia itaongezeka ikiwa watakuwa wakipewa chakula shuleni.

Aliongeza, “Mambo yakiwa mabaya sana, huwa tunagawa chakula chetu na kuwapa wanafunzi. Lakini hata hilo halisaidii kwa sababu idadi ya wanafunzi wanaokabiliwa na baa la njaa ni wengi sana.

“Unakuta katika darasa moja zaidi ya wanafunzi 10 hawana chakula. Inakuwa vigumu kuwafaa wote kwani ni jambo la kila siku.”

Wengi wa watoto hao hutegemea mlo mmoja pekee kwa siku, ambao wanakula usiku tu wala hawana uwezo wa kumudu kiamsha-kinywa ama chakula cha mchana, walieleza walimu.

 

Damu imepungua mwilini

“Watoto hawa wanazidi kudhoofika siku baada ya nyingine. Visa vya upungufu wa damu mwilini vimeenea kote kwa sababu ya utapiamlo,” akasema mwalimu mwingine ambaye hakutaka jina lake lichapishwe.

Baadhi ya wanafunzi wamegeukia kula maembe huku wengine wakiminya limau na kunywa maji yake ili kupunguza makali ya njaa, mwalimu mwingine aliambia Taifa Jumapili.

Mwaka 2017, kaunti hiyo ilikabiliwa na moja ya vipindi vibaya sana vya ukame kuwahi kutokea katika miaka ya hivi karibuni huku masomo yakisitishwa katika shule kadhaa kwa sababu ya njaa iliyozuka.

Mkurugenzi wa Elimu wa Kaunti, Bi Brigit Wambua ameomba serikali na mashirika ya misaada ya kibinadamu kama Red Cross ziingilie kati kuwasaidia.

 

Wazazi wajumuishwe

“Suala hili haliko chini ya usimamizi wangu lakini wakuu wa shule pia wanafaa kuwajumuisha wazazi ili kupata suluhisho,” Bi Wambua alisema.

Mkurugenzi huyo pia alitoa changamoto kwa wazazi kuwajibika zaidi na kutimiza mahitaji ya watoto wao akisema baadhi wametelekeza majukumu yao.

Taarifa za kuathirika kwa masomo katika baadhi ya shule za Kwale zinatokea huku ripoti kwamba kaunti hiyo inakabiliwa na baa sugu la njaa zikichipuka.

Hii ni kulingana na tathmini ya hivi punde kuhusu usalama wa chakula Kwale baada ya msimu wa mvua fupi mwishoni mwa mwaka jana. Kaunti hiyo ilikabiliwa na ukame mkali 2017.

Tathmini hiyo iliyofanywa na Kamati Elekezi kuhusu Usalama wa Chakula Kenya (KFSSG) pamoja na Mamlaka ya Kitaifa ya Kukabiliana na Majanga (NDMA), inatoa picha ya kuogofya kuhusu hali ya chakula katika kaunti hiyo.

Serikali ilitangaza Ijumaa mipango ya kutumia Sh3.8 bilioni kusaidia wananchi wanaokabiliwa na njaa.