Wakuu wa shule wataka ruhusa watoze wazazi ada ya kujenga madarasa
JOSEPH WANGUI na WANDERI KAMAU
WAKUU wa shule za upili katika eneo la Kati wamemwomba Waziri wa Elimu Bi Amina Mohamed kuwaruhusu kuwatoza wazazi ada ndogo ili kuwawezesha kujenga madarasa na mabweni katika shule zao.
Aidha, hili linatokana na idadi kubwa ya wanafunzi ambao wamejiunga na Kidato cha Kwanza.
Kupitia Chama cha Walimu Wakuu wa eneo la Mlima Kenya (MTF), walimu hao walisema kwamba uwepo wa idadi kubwa ya wanafunzi umesababisha msongamano mkubwa sana katika madarasa na mabweni katika taasisi hizo.
“Nafasi iliyopo haiwatoshi wanafunzi hao. Pia, fedha tulizo nazo ni kidogo sana kutuwezesha kushughulikia idadi kubwa ya wanafunzi,” akasema Bw Ndung’u Wangenye, ambaye ndiye mshirikishi mkuu wa chama hicho.
Alitoa mfano wa shule moja ya upili ya wavulana mjini Thika, ambayo ililazimika kubadilisha jumba lake la maakuli kuwa la bweni ili kutosheleza idadi kubwa ya wanafunzi.
Alisema kuwa baadhi ya shule pia zimelazimika kubadilisha maabara na afisi za walimu kuwa madarasa.
Kwingineko, Naibu Rais William Ruto ametoa onyo kwa shule za upili za kutwa ambazo zinawatoza wanafunzi karo.
Bw Ruto alisema kuwa hakuna mtu yeyote anayepaswa kuitisha fedha zozote kutoka kwa wanafunzi, kwani serikali inashughulikia gharama zote.
Akizungumza katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Milo katika eneobunge la Webuye Magharibi Jumamosi, Bw Ruto alisema kuwa serikali imejitolea kuwalipia karo wanafunzi wote, bila kujali wanakotoka.