Habari Mseto

Kenya sasa yaomba Benki ya Dunia Sh75 bilioni

May 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU 

Kenya imeomba mkopo wa mabilioni ya pesa kutoka kwa Benki ya Dunia ili kufadhili bajeti yake, ikisema kuna miradi ya dharura inayohitaji fedha.

Hii ni ishara ya changamoto za kifedha zinazoikumba serikali kutokana na kudidimia kwa mapato na kuongezeka kwa madeni.

Taifa Leo Dijitali imebaini kuwa Benki ya Dunia itafanya uamuzi ikiwa itaipa Kenya Sh75 bilioni.

Aina ya mkopo ulioombwa na Kenya hutolewa kwa haraka ambapo fedha huingia moja kwa moja kujazilia bajeti.

Chini ya usimamizi wa Mwai Kibaki, Kenya ilikataa aina hii ya mkopo ambapo badala yake Benki ya Dunia ilikuwa ikifadhili miradi ya maendeleo.

Ombi hilo lilikuwa ni kupitia kwa barua iliyoandikiwa Rais wa Benki ya Dunia Kristalina Georgieva na Waziri wa Fedha Henry Rotich, Machi 13, 2019.

Katika ombi hilo, Rotich alisema serikali ilihitaji fedha hizo kufadhili miradi ya Ajenda Nne Kuu za serikali.

Kulingana na ombi hilo ambalo liliwekwa kwenye tovuti ya benki hiyo, fedha hizo zitatumiwa kufadhili nyumba za bei rahisi, kuimarisha mapato ya wakulima, usalama wa chakula na miradi ya maendeleo.

Lakini ombi hilo halielezi miradi kamili itakayofadhiliwa, na kuacha nafasi ya kufadhili shughuli za kisiasa au kuibwa na baadhi ya watu, hasa wanasiasa wafisadi.

Taifa Leo Dijitali imebaini kuwa ombi hilo linapingwa na baadhi ya mataifa yaliyo na wawakilishi katika bodi ya Benki ya Dunia.

Kulingana nao, kutokana na changamoto za usimamizi wa fedha za umma Kenya na ukosefu wa uwazi katika matumizi ya mapato, hasa Eurobond, mkopo huo haufai Kenya.