Madiwani 9 kukosa vikao kwa kuzua fujo
Na ANITA CHEPKOECH
MADIWANI tisa wa Bunge la Kaunti ya Kericho wamesimamishwa kushiriki katika shughuli za kamati mbalimbali huku wengine watatu wakitakiwa kuomba msamaha kufuatia vurugu zilizozuka bungeni mnamo Januari 5.
Madiwani walipigana baada ya kutofautiana kuhusu mradi wa Sh100 milioni wa uwanja mdogo wa ndege wa Kerenga.
Kamati ya Nidhamu inayoongozwa na Dominic Rono Ijumaa iliwasilisha ripoti iliyotaka madiwani waliozua vurugu waadhibiwe.
Madiwani Albert Kipkoech (Soliat) na Erick Bii (Maalumu) waliadhibiwa kwa kusimamishwa kuhudhuria vikao 16 vya kamati. Wawili hao wanadaiwa kubeba fimbo ya mamlaka ya bunge na kuitupa nje kupitia dirishani wakati wa vurugu hizo.
Madiwani wengine saba wakiongozwa na Paul Chirchir (Kapsoit) ambaye alipinga vikali hatua ya Gavana Paul Chepkwony kutaka kukarabati uwanja wa Kerenga, walipigwa marufuku kuhudhuria vikao 14 vya kamati zao kwa kupanga na kuchochea vurugu hizo.
Wendani wa Gavana Chepkwony; Collins Byegon (Kapkugerwet), Aron Rotich (Cheptororiet/Seretut) na Anne Tanui (Maalumu) walitakiwa kuandika barua rasmi ya kuomba radhi kwa Bunge la Kaunti ndani ya siku tatu.
Adhabu hiyo ilitolewa siku tatu baada ya Spika wa Bunge, karani Martin Epus na mkuu wa usalama kualikwa kwenda kuandikisha taarifa kwa Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC) mjini Nakuru.
Wengine waliopata mwaliko wa kuandikisha taarifa mnamo Januari 29 ni Naibu Spika Josphat Ruto, Bw Chirchir, Bw Kipkoech na Bw Bii.
Katika mwaliko wake, Mkuu wa EACC ukanda wa South Rift Gilbert Lukhoba alisema madiwani hao wanatakiwa kutoa taarifa kuhusiana na vurugu zilizozuka ndani ya Bunge la Kaunti.
Mzozo huo ulizuka huku Gavana Chepkwony akizindua kamati ya kusimamia mradi huo, ambayo inasimamiwa na waziri wake wa Barabara Charles Birech.
Kamati hiyo itasimamia shughuli ya ukarabati wa uwanja huo.
“Uwanja huo una urefu wa kilomita 1.2 na upana wa mita 18. Upana unatarajiwa kupanuliwa hadi mita 23,” akasema Bw Chepkwony.
Alisema Mamlaka ya Safari za Ndege (KCAA) na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (KAA) zinaunga mkono mradi huo.