KNH yarudisha kazini madaktari iliyowasimamisha kazi
Na BERNARDINE MUTANU
HOSPITALI ya Kenyatta (KNH) Alhamisi ilibatilisha barua za kuwasimamisha kazi madaktari wawili walio katika mafunzo na waliohusika katika kisa cha upasuaji wa ubongo wa mgonjwa asiyehitaji wiki iliyopita.
Hospitali hiyo ilichukua hatua hiyo na kuwasihi madaktari wote waliogoma kurudi kazini.
“Bodi imesimamisha kabisa hatua za kinidhamu dhidi ya madaktari hao. Tumeachia jukumu hilo bodi ya chama cha madaktari,” alisema mwenyekiti wa bodi ya KNH Bw Mark Bor wakati wa mkutano wa wanahabari Alhamisi.
Bodi ya KNH ilikutana na KMPDB pamoja na Waziri wa Afya Bi Sicily Kariuki kujadili suala hilo ambalo lilifanya madaktari wote walio katika mafunzo kugoma na kuathiri shughuli za afya hospitalini humo.
Hii ni baada ya daktari aliyehusika katika kisa cha upasuaji wa ubongo, lakini kwa mgonjwa ambaye hakuhitaji upasuaji huo, kusimamishwa kazi na KNH.
“Tunawaomba madaktari kurudi kazini, tunawathamini na kuheshimu kazi yenu,” alisema Bw Bor na kuongeza kuwa bodi hiyo pia itafanya mkutano na Baraza la Wauguzi ili kuafikiana kuhusu wauguzi wawili waliosimamishwa kazi.
Kulingana na Waziri wa Afya Bi Kariuki, kisa hicho kinachunguzwa na shirika la nje na kulitaka kutia juhudi ili kumaliza uchunguzi huo.
“Ninatarajia bodi ya KNH itashirikiana na KMPDB kwa kutoa habari inayohitajika katika uchunguzi,” alisema Bi Kariuki.
Lakini alikataa kuzungumzia suala la Mkurugenzi Mkuu wa KNH Bi Lily Koros, ambaye alimsimamisha kazi kuhusiana na suala hilo.
Kusimamishwa kazi kwa Bi Koros kumezua mjadala mkubwa wa kisiasa, suala ambalo mwenyekiti wa KMPDB Prof George Magoha alisema hangeingilia.
“Kutoka kwa bodi, tunataka madaktari kurejea kwa sababu hatutaki kuwa na vifo vinavyoweza kuepukika,” alisema, na kutoa ombi kwa KNH kubatilisha barua dhidi ya daktari aliyehusika.
“Tumepokea faili zote zilizo na ripoti kuhusiana na suala hilo, tunataka kurejea kwa madaktari kurejea kwa nia nzuri, tunataka kufanya haki kwa sababu lazima wahusika wasikilizwe,” alisema Prof Magoha.