• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
Usalama mkali kongamano la walimu wakuu likianza

Usalama mkali kongamano la walimu wakuu likianza

Na WINNIE ATIENO

USALAMA umeimarishwa eneo la Pwani huku zaidi ya walimu wakuu zaidi ya 9,000 wa shule za sekondari za umma wakianza kongamano lao la kila mwaka mjini Mombasa.

Mkutano huo unajiri huku shule za umma zikikabiliwa na changamoto tele zikiwemo za kifedha.

Walimu hao watakusanyika katika ukumbi wa Taasisi ya Ushuru nchini (KESRA) iliyoko eneo la Nyali katika barabara kuu ya Mombasa-Malindi. Warsha hiyo ya 44 itaanza Jumapili hadi Ijumaa.

Leo, kamati andalizi itaeleza mada muhimu ambayo itashughulikiwa katika mkutano huo.

Mnamo Ijumaa, wakuu wa usalama wa eneo la Pwani na kamati hiyo ikiongozwa na mwenyekiti wa muungano wa walimu wakuu (Kessha) Bw Indimuli Kahi, walikutana kujadili usalama na mkutano huo.

“Mipango yote imewekwa kuhakikisha usalama unadumishwa katika ukumbi wa mkutano na viunga vyake. Suala la trafiki pia limeshughulikiwa,” alisema kamanda wa polisi wa Mombasa Bw Johnston Ipara.

Imara

Alisema maafisa wa polisi watashika doria kila eneo na wako imara endapo kutakuwa na tisho lolote la usalama.

“Tumewahakikishia usalama wao na hata wakazi wa Mombasa,” aliongeza kamanda huyo.

Kati ya mada tata ambazo zitajadiliwa ni pamoja na mtaala mpya, miundombinu iliyozorota katika shule za umma, ukosefu wa fedha na msongamano katika shule za bweni.

Chama cha walimu pia kitatumia fursa hiyo kuitaka Tume ya Walimu kueleza bayana kwa nini walimu 280 walisimamishwa kazi kwa kupinga mtaala huo.

Wazazi nao wanataka suala la walimu kunyemelea wanafunzi lijadiliwe kwa kina ikiwemo mimba za wanafunzi.

Kinyume na miaka mingine, mwaka huu warsha hiyo itafanyika katika ukumbi wa taasisi ya mafunzo ya ushuru badala ile ya Wild Waters.

Mwenyekiti wa kamati ya usalama Evans Achoki alisema waandalizi walibadilisha ukumbi kwa sababu ya nafasi.

You can share this post!

MWANASIASA NGANGARI: Kiongozi aliyetimua Jaramogi kupitia...

Ruto kusaidia familia ya mtoto aliyegongwa na msafara wake

adminleo