• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:10 PM
Dhamana ya Sh1m kwa kuiba simu na ‘kufuliza’ Sh150,000

Dhamana ya Sh1m kwa kuiba simu na ‘kufuliza’ Sh150,000

Na JOSEPH WANGUI

MWANAMUME aliyeshtakiwa kwa madai ya kuiba simu za watu wanaovinjari vilabuni na kutumia laini zao kukopa pesa kutoka kwa huduma za mikopo kidijitali, ameachiliwa kwa dhamana ya Sh1 milioni.

Bw Nelson Kamau alifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Nyeri, Bi Wendy Kagendo akashtakiwa kwa makosa matatu ya wizi na kujifanya kuwa watu wengine.

Alikamatwa na majasusi waliokuwa wakimsaka kwa miezi mitatu.

Mahakama iliambiwa kwamba mnamo Aprili 18, Bw Kamau aliiba simu aina ya iPhone inayogharimu Sh80,000 kutoka kwa Bw Fredrick Omondi katika baa ya Tenth Street iliyo mjini Nyeri.

Kulingana na hati ya mashtaka, Bw Kamau alitoa Sh43,000 kutoka kwa akaunti ya M-Pesa za Bw Omondi, akaomba mkopo wa Sh90,000 kutoka Stima Sacco na mkopo mwingine wa Sh11,000 kutoka kwa programu ya kutoa mikopo kidijitali ya Timiza.

Mahakama pia ilielezwa mshtakiwa aliomba mkopo mwingine wa Fuliza wa Sh11,500 kwa kutumia simu hiyo hiyo.

Kwenye shtaka la pili, hati ya mashtaka ilisema mnamo Februari 23, aliiba simu ya mkononi aina ya Nokia iliyogharimu Sh28,000 kutoka kwa Bw Bernard Wanjohi katika baa hiyo.

Ilisemekana Bw Kamau alitoa Sh8,000 kutoka kwa akaunti ya M-Pesa ya Bw Wanjohi akachukua mikopo miwili ya Sh2,000 na Sh3,500 kutoka kwa huduma za M-Shwari na Fuliza, mtawalia. Alikumbwa na shtaka la tatu la kujifanya kuwa watu wengine.

Mahakama iliambiwa mshtakiwa alikuwa na kitambulisho cha kitaifa chenye jina John Gachuki Ndirangu, ambayo si jina lake. Kesi hiyo itaendelea mnamo Juni 18.

Bw Kamau alilalamikia korti kwamba gari lake la kibinafsi na simu zake zimezuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Nyeri, akaomba mahakama iagize ziachiliwe.

Mahakama ilimwambia arejelee maswala hayo wakati kesi itakaporudiwa kwani huenda gari na simu hizo ni sehemu ya ushahidi utakaotumiwa na upande wa mashtaka.

You can share this post!

Kuria ashangaa handisheki bado haimtoi kortini

Yashukiwa mwanafunzi alikufa kwa kupigwa shuleni

adminleo