• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Wakazi Mlima Elgon wataka kafyu ya siku 90 iondolewe

Wakazi Mlima Elgon wataka kafyu ya siku 90 iondolewe

Na DENNIS LUBANGA

WAKAZI katika eneo la Mlima Elgon, Kaunti ya Bungoma sasa wanaitaka Serikali kuondoa kafyu ya siku 90 ambayo imewekwa ili kukabili hali ya ukosefu wa usalama katika eneo hilo.

Aidha, walidai kwamba polisi wamekuwa wakiwahangaisha na kupora mali yao kwa kisingizio cha kuwakabili wahalifu.

Kafyu hiyo iliwekwa na Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i wiki tatu zilizopita.

“Polisi hao huwa wanaitisha pesa kutoka kwa yeyote wanayekutana naye barabarani usiku. Wale walioathirika zaidi ni wahudumu wa bodaboda. Licha ya kulipa ada zao wanazotakiwa, fedha kidogo ambazo huwa wanapata huwa zinachukuliwa nao, hali inayotufanya kushangaa ikiwa waliletwa kutulinda ama kutuhangaisha,” akasema Bw John Wanyama, ambaye ni mkazi wa Kipsion.

Baadhi ya wakazi waliozungumza na ‘Taifa Leo’ walisema kwamba licha ya hali ya utulivu kurejea katika eneo hilo, hali ya kibiashara ingali kuimarika.

Eneo hilo limekuwa likishambuliwa na magenge ya uhalifu kutoka mlima huo, hali inayoaminika kuchochewa na mizozo ya ardhi.

“Tunamwomba Dkt Matiang’i kumaliza kafyu hii kwa kuwa baadhi yetu tunaofanya biashara hatuwezi kuendesha kazi zetu kutokana na vitisho vya polisi. Baadhi ya wakazi pia hawawezi kurejea mashambani mwao,” akasema Bi Salina Nechesa, ambaye ni mkazi wa eneo la Masaek.

Mbali na hayo, wakazi pia wanaitaka serikali kuwahamisha baadhi ya polisi ambao wamekaa sana katika eneo hilo.

“Ukweli ni kwamba baadhi ya polisi ambao wamekaa sana katika eneo hili wamezoeana na wakazi. Hilo linamaanisha kuwa hakuna lolote muhimu wanaweza kufanya ili kurejesha hali ya usalama. Wanapaswa kuhamishwa na polisi wengine wapya kuletwa,” akasema Bw Nelson Ndiema, ambaye ni mkazi.
Viongozi wa eneo hilo pia wametoa kauli kama hizo.

“Kuna hitaji lipi la kafyu hii, ilhali tuna mpango wa Nyumba Kumi? Uwepo wa kafyu hii unaathiri sana hali ya uchumi. Polisi hao wanawapunja wakazi kwa kuwaitisha pesa,” akasema Seneta Moses Wetang’ula.

Mwakilishi wa Wanawake katika kaunti hiyo Bi Catherine Wambilianga pia alisema kuwa kafyu hiyo inapaswa kuondolewa.

You can share this post!

Mkutano wa Uhuru na Raila wazidi kusifiwa

TAHARIRI: Mvua iwe baraka kwa hatua zifaazo

adminleo