Polisi wafurika mitandaoni kuelezea masaibu yao
Na VALENTINE OBARA
MAAFISA wa polisi wamegeukia mitandao ya kijamii kulalamikia mazingira hatari ya kazi huku wakiwasuta wakubwa wao moja kwa moja kwa kuwapuuza.
Idara ya Polisi nchini ni mojawapo ya vitengo vya kiserikali ambavyo maafisa huhitajika kutii amri bila maswali, na hivyo hatua ya baadhi yao kwenda kinyume na matarajio haya inashangaza wengi.
Jumatano, Bw Patrick Safari, ambaye ni askari jela, alifikishwa mahakamani pamoja na mwanablogu Robert Alai kwa madai kwamba walishirikiana kusambaza picha za maafisa waliouawa Wajir.
Polisi wanasema usambazaji wa picha hizo ulikuwa sawa na kushabikia ugaidi.
Kwa muda mrefu, Bw Safari, ambaye ana ufuasi mkubwa kwenye mitandao ya kijamii, amekuwa akitoa maoni yake bila uwoga kuhusu masuala tofauti ya kitaifa ikiwemo siasa na usimamizi wa polisi.
Wakati mwingine, yeye huchapisha picha zake akiwa amevalia sare za kikazi na kubeba bunduki huku akieleza anavyoenzi kazi yake ya ulinzi.
Wakati shambulio la Al-Shabaab eneo la Wajir lilipotokea na kusababisha vifo vya polisi 13 wiki iliyopita, alikuwa miongoni mwa walioibua suala kuhusu magari ya kustahimili vilipuzi ambayo yalizinduliwa na Rais Uhuru Kenyatta mnamo 2017.
Alidai idadi kubwa ya magari hayo hayawezi kutumiwa kwa sababu hayana magurudumu na mafuta, ndiposa polisi wanatumia magari ya kawaida katika maeneo yenye hatari ya vilipuzi.
“Maafisa 13 wa polisi walifariki na hadi sasa hakuna mkuu yeyote wa polisi ambaye amezungumza. Ni kana kwamba kila kitu kiko shwari. Ni lini mtu atajitokeza kuwafuta kazi wale wanaohusika na utepetevu huu ambao unasababisha vifo vya maafisa?” akauliza askari huyo wa magereza.
Jumanne, muda mfupi kabla ya kufichua kwamba alipokea habari kuwa polisi wanataka kumkamata, alishangaa kwa nini Bw Alai alikamatwa.
Aliandika: “Nina hakika picha hizo hazikutoka kwake. Lazima zilitoka kwa afisa wa polisi mwenye hasira aliyehusika kwenye operesheni hiyo. Walizisambaza ili kufichua uozo uliopo kwenye idara na kuonyesha masikitiko yao.”
Kando na Bw Safari, afisa mwingine wa polisi aliye miongoni mwa wanaokosoa idara hiyo mitandaoni ni aliyekuwa Naibu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kusimamia Majanga Kitaifa (NDMU), Bw Pius Masai.
Mbali na kulalamika kibinafsi kuhusu hali mbaya ya idara hiyo, Bw Masai huchapisha malalamishi ya maafisa wengine ambao wanahofia kujitokeza wazi.
“Wakati raia wa kawaida anapowasilisha malalamishi, matokeo hutakikana mara moja. Mbona ripoti zinazowasilishwa nasi maafisa wa polisi zinapuuzwa? Kwani sisi si binadamu?” akasema.
Lakini Msemaji wa Polisi, Bw Charles Owino alipuuzilia mbali lalama kwamba kuna utepetevu na usimamizi mbaya katika idara ya polisi, akisema serikali imejitahidi sana kuboresha hali ya utoaji huduma za usalama kitaifa.