• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 12:46 PM
Wakulima wote nchini kusajiliwa kuzima maajenti walaghai

Wakulima wote nchini kusajiliwa kuzima maajenti walaghai

Na STANELY KIMUGE

SERIKALI itawasajili wakulima wote nchini, ili kuondoa mawakala ghushi katika sekta hiyo, amesema Waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri.

Waziri alisema kwamba mfumo huo utahakikisha kwamba ni wakulima halisi pekee, ambao wananufaika kupitia mipango mbalimbali ya serikali, hasa katika upunguzaji bei wa bidhaa mbalimbali.

“Tumepokea malalamishi mengi, hasa kuhusu usambazaji wa mbolea ya bei rahisi inayotolewa na serikali. Mojawapo ya malalamishi hayo ni kwamba haiwafikii wakulima,” akasema.

Akaongeza: “Utoshelevu wa vyakula ni mojawapo ya ajenda kuu za serikali ya Jubilee. Serikali imejitolea kabisa kuhakikisha kwamba imewasaidia wakulima kuongeza uzalishaji maradufu.”

Alisema kwamba mpango huo utahakikisha kwamba wakulima katika sekta zote, ikiwemo ufugaji, wamejumuishwa.

Mapema wiki hii, magunia kadhaa ya mbolea maalum ya serikali yalinaswa mjini Kakamega yakiwa yamepakiwa tayari kuuzwa.

“Tutaanza hatua kali dhidi ya afisa yeyote wa serikali ambaye atapatikana akishiriki katika uuzaji wa mbolea kinyume cha sheria,” akasema.

Alisema kwamba wakulima ambao watawasilisha mahidi yao katika mabohari ya Halmashauri ya Kitaifa ya Kununua Nafaka (NCPB) watapewa mbolea, huku wakingoja kulipwa fedha zao.

“Tutahakikisha kwamba tutawasilisha bidhaa hizo kwa wakulima hao kupitia vyama vyao vya ushirika,” akasema Bw Kiunjuri.

Wakulima katika ukanda wa Bonde la Ufa wameanza kununua mbolea hiyo kwa Sh1500 kwa gunia la kilo 50. Hilo ni ikilinganishwa na Sh1800 mwezi uliopita.

Hata hivyo, baadhi ya mawakala ghushi wameingilia usambazaji wa mbolea hiyo, ambapo wamekuwa wakiipakia kwa mifuko midogo midogo. Baadaye, huwa wanaiuza kwa bei za kati ya Sh2500 na Sh4000.

Kwa hayo, waziri alisema kwamba serikali inawarai wakulima kuhifadhi maji msimu huu wa mvua, ili kuhakikisha hakuna upungufu wa vyakula wakati wa kiangazi.

“Mikakati tunayofanya ni kuhakikisha kuwa hakuna upungufu wowote wa vyakula unaotokea wakati wa kiangazi,” akasema Bw Kiunjuri.

Mbali na hayo, alisema kuwa serikali inafanya kila iwezalo kukabili viwavi ambao wamekuwa wakivamia na kuharibu mahindi.

Bw Kiunjuri alikuwa akihutubu katika Maonyesho ya Kitaifa ya Kilimo ya Eldoret, ambayo kaulimbiu yake kuu ni uimarishaji wa teknolojia katika kilimo.

 

 

You can share this post!

Uhuru aagiza polisi waliohudumu kwenye Uchaguzi Mkuu...

Sakata mpya ya mahindi serikalini yawaletea wakulima hasara...

adminleo