Michezo

Kenya yaibuka na shaba michezo ya ufukweni

June 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

KENYA ilikamilisha mashindano ya Bara Afrika ya ufukweni kwa kushinda nishani ya shaba katika voliboli ya wanawake yaliyofika tamati mjini Sal nchini Caper Verde.

Ushirikiano wa Gaudencia Makokha na Naomie Too ulinyamazisha wenyeji Janice Varela na Ludmila Varela kwa seti 2-0 za alama 21-6, 21-11 katika mechi ya kutafuta nambari tatu iliyodumu saa moja.

Wakenya walikamilisha kitengo hiki na ushindi tano kati ya mechi sita ilizocheza. Ilichapa Sierra Leone, Guinea-Bissau na Nigeria kwa seti 2-0 kila mmoja kabla ya kupokea dozi sawa na hiyo kutoka kwa Namibia katika nusu-fainali Juni 22. Ilijikakamua na kuzidia wanavisiwa wa Cape Verde katika mechi ya kutafuta medali ya shaba.

Ilimaliza soka katika nafasi ya sita baada ya kulimwa 10-6 na Algeria.

Katika mbio za kilomita 21, Charles Yosei Mneria alimaliza wa pili nyuma ya Robert Chemonges (Uganda) na mbele ya raia wa Djibouti Bouh Moumin kwenye kitengo cha wanaume naye Florence Malyunga akiridhika katika nafasi ya nne nyuma ya Senani Reham (Algeria), Lavinia Haitope (Namibia) na Priscilla Chelangat (Uganda) kwa upande wa wanawake.

Katika makala haya ya kwanza, Kenya pia ilizoa medali ya shaba katika tenisi ya wachezaji wawili kila upande kupitia kwa Fazal Khan na Ibrahim Yego. Kenya iliambulia pakavu katika fani za ‘kiteboarding’, kupeleka mashua kwa kutumia mitumbwi, karate, soka, handboli na uogeleaji.