Serikali yatetea SRC dhidi ya vitisho vya wabunge
Na VALENTINE OBARA
SERIKALI Kuu imetetea Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) dhidi ya wabunge wanaotaka kupunguzia tume hiyo fedha za kuendeleza shughuli zake mwaka huu.
Waziri wa Fedha, Bw Henry Rotich amesema SRC ina jukumu muhimu katika kusaidia serikali kupunguza gharama ya mishahara ya watumishi wa umma iliyopita Sh730 bilioni mwaka uliopita, ili fedha zitumiwe zaidi kwa miradi ya maendeleo na kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.
Akizungumza Alhamisi wakati tume hiyo ilipozindua mwongozo wa utendakazi wake katika kipindi cha mwaka wa 2019 hadi 2024 jijini Nairobi, Bw Rotich alisema majukumu ya kikatiba ya SRC hayafai kutatizwa.
Majukumu hayo yanajumuisha kuhakikisha gharama ya mishahara ya watumishi wa umma si ya juu kupita kiasi, na watumishi wa umma wanalipwa mishahara inayolingana na kazi wanazofanya.
“Ninawahakikishia kwamba tutashauriana na bunge wakati wote ili mpate rasilimali zote mlizotengewa kufanya kazi yenu,” akasema Bw Rotich.
SRC inayosimamiwa na Bi Lyn Mengich ilipata pigo wiki iliyopita wakati Bunge la Taifa lilipoipunguzia bajeti yake kwa Sh95 milioni. Wakati huo, tume hiyo ilikuwa imetengewa Sh545.4 milioni kwenye bajeti na kabla ya hapo, ilikuwa imetengewa Sh645.4 milioni kabla wabunge kukata kiwango hicho kwa Sh125.6 milioni.
Hatua hizo zilionekana kama njia ya wabunge kulipiza kisasi kwa jinsi SRC ilivyopinga mahakamani uamuzi wao wa kujilipa marupurupu ya nyumba ya Sh250,000 kila mwezi.
Mojawapo na mikakati inayolengwa kutekelezwa na SRC kupunguzia Wakenya gharama ya kulipa mishahara ni kama vile kuajiri watumishi wa umma kwa kandarasi kabla kuamua iwapo wanastahili kupandishwa vyeo kwa kuzingatia utendakazi wao.
Bw Rotich alitaka tume hiyo ihakikishe mikakati yoyote itakayotumiwa kupunguza gharama ya mishahara ifanywe kwa njia ambayo haitaepusha wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu kutafuta kazi serikalini wakihofia hawatalipwa vyema.
“Mapendekezo yatahitaji kuhakikisha tunapopunguza gharama ya mishahara, bado serikali itaendelea kuvutia na kudumisha watumishi wa umma wenye utaalamu wa hali ya juu. Mataifa yaliyofanikiwa kutekeleza mfumo aina hii yalilazimika kuchukua hatua kali hasa katika kubadilisha muundo wa serikali na mashirika ya umma,” akasema.
Alitoa wito kwa wizara zote na mashirika ya umma kushirikiana na SRC ili kufanikisha malengo yake ndipo serikali ipate fedha za kutosha kutekeleza mipango ya maendeleo.