• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
Sonko avuruga maji ngome ya Mutua

Sonko avuruga maji ngome ya Mutua

Na STEPHEN MUTHINI

KULITOKEA kioja mjini Machakos Alhamisi asubuhi wakati Gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko alipoenda katika kituo cha polisi cha Machakos kulalamikia kukamatwa kwa wafanyakazi wa hoteli ya aliyekuwa mbunge wa Kibwezi Kalembe Ndile.

Wafanyakazi hao wa Hoteli ya Macha Beach walikamatwa na maafisa wa Serikali ya Kaunti ya Machakos mnamo Jumatano jioni baada ya Bw Ndile kuandaa kikao cha wanahabari kukashifu jinsi Gavana Alfred Mutua alivyoahidi kukarabati sanamu za mashujaa wa uhuru zilizo Nairobi.

Bw Sonko aliwasili kituoni akiandamana na wabunge kadhaa pamoja na kikosi chake cha Sonko Rescue Team kilichojumuisha watoaji huduma za kwanza za matibabu ambao pia walibeba vyakula.

“Kalembe alimkosoa gavana kwa njia nzuri. Kama gavana Mutua alikasirishwa na Kalembe angemkamata badala ya wafanyakazi wake,” akasema Bw Sonko.

Serikali ya kaunti hiyo ilisema hatua zilichukuliwa dhidi ya hoteli hiyo kwa kuhudumu bila leseni halali, kukosa mbinu za utupaji taka zinazostahili na wapishi kukosa vyeti vya afya.

Dkt Mutua alikuwa amezuru Nairobi mapema wiki hii na kudai sanamu za mashujaa wa uhuru Tom Mboya na Dedan Kimathi zilitelekezwa.

“Nilimwambia Mutua atoe huduma alizoahidi wakazi wa Machakos badala ya kutumia pesa kupaka rangi sanamu zilizo Nairobi. Baadaye jioni alifunga hoteli yangu na kukamata wafanyakazi,” Bw Ndile akasema.

You can share this post!

Serikali yatetea SRC dhidi ya vitisho vya wabunge

Maisha ya Gakuru yangeokolewa, asimulia dereva

adminleo