• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:55 AM
Watu 40 wauawa kwenye mapigano mapya ya kikabila nchini DRC

Watu 40 wauawa kwenye mapigano mapya ya kikabila nchini DRC

Na MASHIRIKA

KINSHASA, DR CONGO

KARIBU watu 40 wameuawa kaskazini mwa DRC Congo, siku mbili zilizopita kwenye mapigano makali ya kikabila kati ya jamii za Hema na Lendu, zimeeleza ripoti.

Mapigano hayo yamekuwa yakiendelea katika mkoa wa Ituri, kati ya jamii hizo mbili hasimu. Jamii ya Hema huwa wafugaji huku Walendu wakiendeleza kilimo.

Kulingana na Jean Bosco Lalu, ambaye ni kiongozi wa shirika moja lisilo la serikali, huenda idadi hiyo ikaongezeka, kwa kuwa juhudi za kudhibiti mapigano hayo hazijafua dafu.

Afisa mmoja wa serikali alisema kwamba walikuwa wamehesabu miili ya watu 30.

“Kuna uwezekano wa kuwepo kwa miili mingine vichakani. Tungali tunaendelea na uchunguzi wetu,” akasema Willy Maese, aliye Naibu Kamishna Mkuu wa mkoa huo.

Aidha, aliongeza kwamba mamia ya makazi yalichomwa moto kwenye shambulio dhidi ya vijiji viwili mnamo Jumapili.

Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa (UN), zaidi ya watu 130 wameuawa katika eneo la Ituri, tangu mapigano hayo kuanza mnamo Desemba.

Ripoti zinasema maelfu ya watu wametoroka mapigano hayo, ambapo 27,000 kati yao walikisiwa kuingia nchini Uganda. Mwanzoni mwa mwezi uliopita, maelfu ya watu walionekana wakitorokea Uganda kupitia Ziwa Albert kwa kutumia mashua. Kulikuwa na ripoti kwamba zaidi ya nyumba zingine zaidi ya 1,000 zilichomwa wikendi iliyopita katika eneo la Djugu, mkoani humo.

Kuzuka upya kwa mapigano hayo kunaibua kumbukumbu ya mapigano mengine yaliyodumu kati ya 1998 na 2003 kati ya jamii hizo mbili, ambapo maelfu ya watu wanadaiwa kuuawa.

Mnamo 2017, ghasia hizo zilichangia watu zaidi ya 1.7 milioni kutoroka makwao. Licha ya kimya chake, Uganda imekuwa ikilaumiwa kwa kuwa mchochezi mkuu wa mgogoro huo. Shirika la Human Rights Watch limeilaumu kwa kuwapa mafunzo wapiganaji wa jamii hizo mbili.

Kulingana na shirika hilo, wapiganaji hao baadaye hujiunga na kundi la Congolese Rally for Democracy-Liberation Movement (RCD-ML) ambalo limekuwa likipigania kujitenga kwa sehemu ya mashariki ya taifa hilo. Kundi hilo huwa linaungwa mkono na Uganda.

Mashirika mbalimbali ya kimataifa yamezilaumu jamii hizo mbili kwa kuwa kikwazo kikuu cha kupatikana kwa mwafaka wa kisiasa.

Mnamo 2006, iliripotiwa kwamba hadi watu 60,000 walikuwa wameuawa, tangu mapigano hayo kuanza mnamo 1998.

Kijumla, inakisiwa kwamba zaidi ya watu 50,000 wameuawa, huku wengine zaidi ya 500,000 wakifurushwa kutoka makwao. Wengi wamelazimika kuwa wakimbizi katika nchi jirani kama Uganda, Rwanda, Burundi na Tanzania.

 

You can share this post!

Mahabusu asimulia kortini alivyopelekwa benki na polisi...

Kenya yaimarika hadi nafasi ya 105 viwango vya FIFA

adminleo