• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 1:15 PM
Tokeni NASA kama nyinyi ni wanaume, ODM yaambiwa

Tokeni NASA kama nyinyi ni wanaume, ODM yaambiwa

Na WYCLIFFE MUIA

BAADHI ya wabunge wa vyama vya Wiper, ANC na Ford Kenya sasa wamewataka wenzao wa ODM waondoke kutoka kwa muungano wa NASA kama hawaoni umuhimu wa upinzani.

Wabunge hao zaidi ya kumi wanawataka vinara wa NASA kuitisha kikao cha wabunge wote wa upinzani, ili kuwaelezea kwa kina mazungumzo kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Wakiongozwa na mbunge wa Lugari Ayub Savula, walisema vyama vyao vitatu viko tayari kuhudumu kama upinzani bungeni iwapo ODM itaungana na chama cha Jubilee.

“Iwapo ODM itaamua kuolewa na serikali nakufanya kazi pamoja, tuko tayari kuwa upinzani rasmi bungeni,” alisema Bw Savula katika hoteli ya Panafric jijini Nairobi.

Bw Savula alisema vyama hivyo vitatu havibanduki NASA na kuonya ODM dhidi ya kudhalilisha wabunge kutoka vyama vingine tanzu vya upinzani.

“Hatutoki NASA. Sisi ni wamiliki wa NASA. Hatutakubali kutishwa na yeyote. Kama ODM wamechoka au wamenunuliwa watuache kwa amani katika upinzani,” aliongeza Bw Savula.

Viongozi hao wanawataka Rais Kenyatta na Bw Odinga kuhakikisha maelewano yao yana misingi ya kisheria, ili kuepuka usaliti wa kisiasa baadaye.

“Sharti vinara wengine wa NASA wajumuishe katika mazungumzo yanayoendelea. Mustakabali wa Kenya hauhusu watu wawili au familia mbili,” alisema mbunge wa Emuhaya, Bw Omboko Milemba.

Naye mbunge wa Makueni, Bw Dan Maanzo aliunga mkono wito wa kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka kutaka wafanye kikao na Rais Kenyatta pamoja na kinara wa Ford Kenya Moses Wetangula na kinara wa ANC Musalia Mudavadi.

“Lengo linapaswa kuunganisha Wakenya wote na wala si viongozi wawili. Wito wa Kalonzo si kukutana tu na rais lakini pia kukumbatia watu wote katika mazungumzo ya kitaifa,” alisema Bw Maanzo.

Lakini akiongea Jumatano baada ya kuhudhuria misa ya wafu ya mwendazake msomi Alloys Tumbo Oeri katika kanisa la Consolata Shrine jijini Nairobi, Bw Wetangula alionekana kutofautiana na Bw Musyoka kuhusu kukutana na Rais Kenyatta.

“Tunapaswa kusahau yale yaliyopita. Tunapaswa kusamehe na kusahau yaliyopita. Sharti tulenge amani na umoja kwa sasa,” alisema Bw Wetangula.

“Bw Odinga, Bw Kalonzo Musyoka, Bw Musalia Mudavadi na mimi ni kama pacha. Tutafanya kazi pamoja kuhakikisha hatuhujumu juhudi hizi za kuunganisha taifa,” akasema Bw Wetang’ula akiongea baadaye katika Bunge la Seneti.

Naye kiongozi wa wengi katika Bunge la Kitaifa Aden Duale vilevile alipuuzilia mbali wito wa Bw Musyoka akisema mkutano wa Bw Odinga na Rais Kenyatta ulitosha kuanzisha mchakato wa umoja nchini.

“Mkutano wa Rais Kenyatta na kinara wa upinzani Raila Odinga hapo Machi 9 ulitosha. Vinara hao wengine ambao sasa wanaitisha mkutano na Rais wanafaa kuunga mkono wawili hawa,” akasema Bw Duale.

 

You can share this post!

MAAFA YA MVUA: Watu tisa waangamia

Ndoa ya NASA yaingia doa: ODM yampiga Wetang’ula...

adminleo