• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Ajabu ya matajiri wa mahindi kumezwa na ufukara

Ajabu ya matajiri wa mahindi kumezwa na ufukara

Na BARNABAS BII

WAKULIMA wengi wa mahindi katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa wanaishi katika hali ya umaskini licha ya kupata mavuno mengi ya zao hilo msimu uliopita.

Wakulima hao, ambao bado wana mahindi ya msimu uliopita, wako katika hatari ya kupata hasara zaidi wanapojitayarisha kuvuna mahindi ya msimu huu miezi mitatu ijayo.

Masaibu yao yanatarajiwa kuongezeka kutokana na hatua ya serikali kupanga kuagiza magunia 12 milioni ya mahindi ambayo yataingizwa nchini bila ushuru.

Aidha, masaibu ya wakulima hawa yameongezwa na watu ambao waliwapa mikopo kununua pembejeo katika misimu miwili iliyopita.

Wengi wao wameshindwa kulipa mikopo kutokana na hatua ya Halmashauri ya Kitaifa ya Ununuzi Nafaka (NCPB) kununua mazao yao kwa bei za chini.

Watu hao wametoa makataa kwa wakulima hao kulipa mikopo la sivyo mali yao ipigwe mnada.

Bw Kipruto Kirwa kutoka kijiji cha Natwana, Kaunti ya Uasin Gishu huwa anakuza mahindi katika shamba lake la ekari 30, ambapo huzalisha magunia 900.

Hata hivyo, anasema kuwa gharama kubwa ya pembejeo kama fatalaiza ni kikwazo kikubwa katika kilimo chake.

Kwa wastani, huwa anatumia Sh6,000 kulima shamba hilo kwa trekta, Sh1,500 kupanda, Sh4,500 kupalilia mahindi, bila kuzingatia gharama zingine kama kuwalipa wafanyakazi.

“Serikali inapaswa kupunguza gharama ya ukuzaji wa mazao kama mahindi, ili kuwawezesha wakulima kudumisha na kuongeza uzalishaji. Hata hivyo, huenda ongezeko la bei kwa pembejeo hizo likawatatiza wakulima wengi,” akasema Bw Kirwa, kwenye mahojiano na Taifa Leo.

You can share this post!

Kanisa lataka vikosi vya polisi vishirikiane kuzima uhalifu

Joyce Akinyi akamatwa tena kuhusu mihadarati

adminleo