• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
Muungano mkuu wa upinzani wanukia nchini Uganda

Muungano mkuu wa upinzani wanukia nchini Uganda

Na DAMALI MUKHAYE

KAMPALA, UGANDA

HARAKATI za kumbandua mamlakani Rais wa Uganda Yoweri Museveni zimepamba moto huku majadiliano kati ya wapinzani wake wawili wakuu ambao ni aliyekuwa mgombea urais Dkt Kizza Besigye na Mbunge Robert Kysangulanyi yakifikia kilele.

Hii ni baada ya kuibuka kwamba mazungumzo kati ya Dkt Besigye na kiongozi wa People Power na mbunge wa Kyadondo Mashariki, Kyagulanyi, maarufu ‘Bobi Wine’, kuhusu mpango wa kuungana pamoja kwa sababu ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2021 yamefikia hatua za mwisho, kulingana na chama cha Opposition Forum for Democratic Change (FDC).

Akizungumza Jumanne na wanahabari katika afisi za makao makuu ya FDC mjini Najjanankumbi, mwenyekiti wa chama Bw Waswa Biriggwa, alisema watatangaza makubaliano kuhusu mazungumzo hayo hivi karibuni.

Vilevile, alisema wawili hao wanafanya kazi kwa pamoja ili kuibandua serikali ya NRM katika uchaguzi ujao.

“Tumekutana mara mbili na kundi la People Power na tutakutana tena kujadiliana kuhusu namna ya kushinda utawala wa sasa. Tutafahamisha umma kuhusu mipango yetu ya mwisho hivi karibuni,” alisema Biriggwa.

“Japo FDC kama chama bado hakijashiriki mazungumzo hayo, Dkt Besigye anayafanya kwa niaba yetu na kama chama, tuko tayari kuungana na makundi mengine yenye malengo sawa,” alisema.

Mnamo Mei, Besigye na Kyagulanyi walianza mikutano isiyo rasmi kuhusu kuungana pamoja kwa lengo la kushinda chama cha National Resistance Movement Party na Rais Museveni, ambaye amekuwa mamlakani tangu 1986.

Mgombea mmoja

Baadhi ya mipango hiyo inajumuisha kumsimamisha mgombea mmoja katika kinyang’anyiro cha urais 2021.

Rais Museveni, ambaye sasa ana umri wa miaka 74, pia anatarajiwa kuwania awamu ya sita ya urais.

Biriggwa pia aliwaeleza wanahabari kwamba, FDC haitajiunga na kundi la Democratic Party (DP) inayoongozwa na Norbert Mao kwa sababu si muungano usioogemea pande maalumu, hivyo hawatajihusisha nao.

“Sawa na jinis ambavyo Bw Mao hawezi kujiunga na FDC, sisi pia hatuwezi kujiunga na DP. Ikiwa wanataka tuungane, acha waunde chama kipya kinachoweza kuruhusu vyama vyote lakini si kundi la DP,” alisema Biriggwa.

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Nilimpendea sauti tu sasa natamani kumuona

Serikali kupimia wazee hewa

adminleo