• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 5:41 PM
KILIMO NA MAZINGIRA: Uchafuzi wa Mto Athi nusra uzime ndoto za mkulima

KILIMO NA MAZINGIRA: Uchafuzi wa Mto Athi nusra uzime ndoto za mkulima

Na SAMMY WAWERU

MEI 2019 kituo kimoja cha runinga kwenye makala ukilifichua uchafuzi wa mazingira Nairobi unavyoathiri Nairobi River, ambao maji yake yamejiunga na Mto Athi.

Mkondo wa Mto Athi umepitia kaunti kadhaa kabla ya kuishia katika Bahari Hindi.

Maji ya mto huu yameathirika pakubwa.

Kwenye ufichuzi ilibainika baadhi ya viwanda na mitaa ya mabanda Nairobi huachilia majitaka kuingia katika mto huo.

Baadhi ya wakulima wanaotegemea Mto Athi kufanya kilimo walilalamika kwamba maji yake yamechafuka kiasi cha kuharibu mimea na mazao.

Isitoshe, viumbe wanaoishi majini kama vile samaki waliripotiwa kupungua na hata wengine kuisha.

Serikali ya kaunti ya Machakos, ulikopitia mto huo, chini ya Gavana Alfred Mutua kwa ushirikiano na halmashauri ya kitaifa ya mazingira, Nema, ilichukua hatua na kufunga baadhi ya viwanda.

Hamasisho la Nema kuhifadhi mazingira

Dkt Mutua alionya kuwa hatafumbia macho suala la uchafuzi wa mazingira na Mto Athi. Nema inaendelea na kampeni yake ya siku 100 kuhamasisha umma umuhimu wa kuhifadhi usafi wa mazingira.

Hamasisho lake linalenga viwanda, majengo ya makazi na mifuko ya karatasi za plastiki iliyopigwa marufuku.

Kulingana na Nema ni kwamba kufikia sasa imezuru zaidi ya makao 1,500, ambapo 300 yamefungwa kwa ukiukaji wa uhifadhi wa mazingira.

Mkurugenzi Mkuu wa halmashauri hiyo Profesa Geoffrey Wakhungu anasema washukiwa 100 wamekamatwa. Idadi hii inajumuisha wanaochafua mazingira kwa kuachilia majitaka ambayo hayajatibiwa na matumizi ya mifuko iliyopigwa marufuku 2017.

“Majitaka yanapaswa kutibiwa kabla kuachiliwa. Ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa,” anasema Profesa Wakhungu.

Anashauri haja ya kuhusisha Nema kabla ya kuachilia majitaka, hili likionekana kulenga viwanda na majengo ya makazi Nairobi. “Maji ya Nairobi River yanategemewa na wengi. Ni yayohayo yanamiminiwa Bahari Hindi, sharti tuhifadhi usafi wake,” anasisitiza.

Kati ya 2010 na 2018, kabla maji ya Mto Athi kuchafuliwa, ungezuru eneo la Joska, lililoko kaunti ya Machakos, ungelakiwa na taswira ya kijani kibichi.

Baadhi ya wakulima walikumbatia mfumo wa kisasa kunyunyizia maji mashamba kwa mifereji, ambapo walizalisha mazao ya aina mbalimbali.

Mkulima kuathirika na uchafuzi wa Mto Athi

Katika shamba la Bw Samuel Mwaniki, lililoko kilomita mbili kutoka Kangundo Road na kilomita 15 hivi kutoka Kamulu, lilikuwa kiunga cha nyanya, kabichi, vitunguu, pilipili mboga na hoho (ile kali), mamumunya na Maharage ya Kifaransa-French beans.

Ana ekari 12, na ni uwekezaji anaosema ulikuwa ukimuingiza mapato lukuki.

“Niliacha kazi kwa sababu kilimo kilinikubali. Nina wateja kutoka Nairobi na Machakos wa mazao niliyozalisha, na kwa sasa hawanitegemei kikamilifu,” Bw Mwaniki akaambia Taifa Leo wakati wa mahojiano.

Aligetemea Mto Athi, ambao u pembezoni mwa shamba lake, kufanya kilimo, na hali kwake si hali tena.

Sababu hasa; ni mmoja wa wakulima walioathirika pakubwa kutokana na uchafuzi wa Nairobi River, ambao mkondo wake wa maji unajiunga na Athi.

Kulingana na mkulima huyu ni kwamba imekuwa vigumu kutegemea mto huo kwani maji yake si salama kufanya kilimo.

“Hayawezi kutumika kulima kwa sababu ya kemikali ya majitaka. Yakinyunyiziwa mimea, kuna inayokauka na inayozalisha si salama kwa afya ya binadamu,” anafafanua Bw Mwaniki.

Kemikali inayotumika katika viwanda vya kuunda bidhaa mbalimbali inapoachiliwa kwenye mto kabla kutibiwa ni hatari kwa viumbe na mimea inayotegemea maji yake.

Ni muhimu kutaja kuwa majitaka ya majengo ya makazi yana uchafu kama sabuni, dawa zenye kemikali zinazopuliziwa kwenye vyoo vya kufyatua.

Kwa kuwa hajakata tamaa katika kilimo, Bw Mwaniki anasema kwa sasa anategemea msimu wa mvua kukuza mimea. Vilevile, huyateka kwa vihifadhio ambapo huyatumia wakati wa kiangazi.

Mkulima huyu anahimiza serikali kupitia asasi husika kama Nema kutolegeza kamba kampeni ya kuhifadhi mazingira.

You can share this post!

NDIVYO SIVYO: Hakuna neno ‘thamana’ katika lugha ya...

SEKTA YA ELIMU: Dhuluma kwa wanafunzi na matumizi ya...

adminleo