• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:24 AM
ODM kumpokonya Jumwa nafasi yake PSC

ODM kumpokonya Jumwa nafasi yake PSC

Na CHARLES WASONGA

HATIMA ya Mbunge wa Malindi Bi Aisha Juma kama kamishna wa Tume ya Huduma za Bunge (PSC) sasa imo hatarini baada ya chama chake, ODM, kutangaza kuwa kitaanzisha mchakato wa kumpokonya nafasi hiyo.

Hii ni kwa sababu Mswada wa Huduma za Bunge uliopitishwa majuzi sasa unatoa utaratibu wa kuondoa mwanachama wa PSC au mbunge ambaye atakaidi misimamo ya chama kilichomdhamini bungeni.

Bi Jumwa amekera chama cha ODM kinachoongozwa na Raila Odinga kwa kutangaza wazi kuwa anaunga mkono azma ya Naibu Rais William Ruto kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Chama hicho kilimpendekeza Bi Jumwa kwa nafasi cha mwanachama wa PSC baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2013. Lakini miezi michache baada ya kuingia katika wadhifa huo, Bi Jumwa alikaidi ODM na kuanza kumpigia debe Dkt Ruto kama anayefaa kumrithi Rais Uhuru Kenyatta atakamilisha muhula wake wa pili na wa mwisho uongozini.

Mbunge huyo , mwenye kipawa cha usemi, amekuwa mstari wa mbele akiendesha kampeni za kuvumisha Dkt Ruto katika mikutano ya hadhara kote nchini, kinyume cha ushauri wa Rais Kenyatta kwa wanasiasa wakomesha siasa za urithi.

Kiranja wa wachache Junet Mohammed Jumamosi aliwaambia wanahabari kwama ataanzisha mchakato wa kumwondoa mbunge huyo mkaidi kutoka tume hiyo ya PSC pindi Rais Kenyatta atakapotia saini mswada huo.

“Ni wazi kuwa Mheshimiwa Jumwa haheshimu sera, maongozi na maono ya chama ambacho kilimteua kuwa mwanachama wa tume ya PSC,” akasema Bw Mohammed ambaye ni Mbunge wa Suna Mashariki.

Kulingana na kipengele cha 14 cha Sheria ya Vyama vya Kisiasa, ya 2012, mwanachama wa chama cha kisiasa ambaye atachukuliwa kuwa amekihama chama hicho endapo anaendeleza masilahi ya chama pinzani.

“Kwa hivyo, kwa sasa Mswada wa Huduma za Bunge unatoa mwongozo na utaratibu wa namna ya kumwadhibu mwanachaama kama huyo, tutafuata utaratibu huo kumwondoa Bi Jumwa kutoka nafasi yake kama mwanachama wa tume ya PSC,” akasema Bw Mohammed ambaye ni mwandani wa karibu wa Bw Odinga.

Mchakato wa kuwaondoa makamishna wa PSC unaongozwa na utaratibu uliotolewa kwenye kipengele cha 127 cha Katiba. Na mnamo Juni mwaka jana chama cha ODM kilianza rasmi kufuata utaratibu wa kumwondoa Jumwa kutoka tume hiyo.

Mnamo tarehe 20 Bw Mohammed alimwandikia barua Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi akielezea nia ya ODM kumpokonya Bi Jumwa nafasi hiyo. Ni ilitokana na hatua ya Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) ya chama hicho kupitisha uamuzi wa kufurusha Mbunge kulingana na mapendekezo ya kamati ya nidhamu iliyompata na hatia ya kukaidi sera za ODM na kudharua viongozi wake akiwemo Bw Odinga.

“Naomba utaratibu kuhusu namna ya kumwondoa kamishna wa PSC… nitashukuru zaidi ikiwa utalishushulikia suala hili kadri ya uwezo wako,” akaandika Bw Mohammed.

Hata hivyo, mchakato huo haungeendelea kwa sasa hakukuwa na utaratibu mahususi wa kisheria wa kuhusu kuondolewa kwa kamishna wa PSC ambaye ni Mbunge.

Mipango ya ODM ilivurugwa hata zaidi kufuatia uamuzi wa Jopo la Kutatua Mizozo ya Vyama vya Kisiasa (PPDT) kusimamishwa kwa muda utekelezaji wa mapendekezo ya kamati yake ya nidhamu, ya kumfurusha Bi Jumwa.

Mswada wa Huduma za Bunge ambao sasa unasubiri sahihi ya Rais Kenyatta inasema kuwa kwa sababu makamishna wa PSC huteuliwa na Bunge kupitia hoja inayowasilishwa na kujadiliwa, Bunge hilo hilo ndilo linapsa kuwa na mamlaka ya kumwondoa kwa njia hiyo hiyo ya hoja inayodhaminiwa na mbunge. Hoja hiyo, kulingana na mswada huo, inaweza kudhaminiwa na Mbunge yeyote yule.

Hii ina maana kuwa chama ambacho kinanuia kumwondoa kamishna wa tume ya PSC sharti kifanye hivyo kupitia hoja iliyowalishwa kwa afisi ya Spika na kuidhishwa kwa mjadala katika vikao vya bunge lote.

Lakini kabla ya Kimati ya Bunge lote kupitisha hoja kama hiyo sharti wabunge waridhike na sababu zilizotolewa na kwamba mlengwa amepewa nafasi ya kujitetea.

Ikiwa mswada huo utatiwa saini ulivyo, Mbunge atakayewasilishwa hoja kwa kumwondoa Kamishna wa PSC sharti apate uungwaji mkono kutoka angalau robo ya wabunge (wabunge 117) ya mabunge yote mawili ili kumwondoa mwanachama huyo kwa sababu zilizoorodheshwa katika kipengee cha 251 cha Katiba.

Ikiwa mswada huo utaungwa mkono na angalau thuluthi moja ya wabunge 349 katika Bunge la Kitaifa au Maseneta 67 katika Seneti, mabunge hayo mawili yatateua kamati ya wanachama 11 kuchunguza masuala yaliyoibuliwa kwenye hoja hiyo.

Kamati hiyo itawasilishwa ripoti yake kwa mabunge hayo mawili baadhi ya kipindi cha siku 10 kuhusu iwapo iliridhika na madai dhidi ya kamishna anayeondolewa. Ikiwa kamati hiyo itabaini kuwa madai hayo hayaafikiwa viwango hitajika, mchakato huo utakomea hapo.

Na ikiwa madai yana mashiko na yanaungwa mkono na wengine wa wanachama wa kamati hiyo ya watu 11 pamoja na wanachama wa bungeni husika, Maspika watasoma rasmi uamuzi huo baada ya siku mbili. Na hapo mwanachama wa PSC atakuwa ameondolewa rasmi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Sheria na Masuala ya Kisheria William Cheptumo anasema kuwa utaribu huo mrefu wa kumwondoa Kamishna wa PSC unanuiwa kudumisha utawala bora na kuzuia matumizi mabaya ya mamlaka.

You can share this post!

Mchezaji azimia uwanjani Oserian wakipiga Kayole Starlets

Faraja shuleni baada ya wanafunzi kuanzisha mradi wa...

adminleo