Polisi 1400 wajiuzulu kwa kupunguziwa mishahara
Na STELLA CHERONO
MAAFISA 1,400 wa polisi wamejiuzulu wakilalamikia hatua ya Tume ya Huduma ya Polisi (NPSC) kupunguza mishahara yao.
Maafisa hao ambao tayari wamepokea mshahara wa Machi waliambia Taifa Leo kwamba mshahara wao umepunguzwa kwa hadi Sh26,000.
Wengi walioathiriwa ni wale walio na digrii na waliolemaa wakiwa kazini ambao walipunguziwa mshahara licha mahakama kuagiza serikali isitekeleze agizo la NPSC ambalo lilitolewa wiki iliyopita.
Kulingana na ilani za mishahara kutoka kwa chama cha ushirika cha Kenya police Sacco, baadhi ya maafisa hao walipata mshahara wa Sh20, Sh50 na Sh150 huku baadhi wakikosa kupata hata senti moja.
Baadhi ya maafisa waliokasirishwa na hatua hiyo tayari wamewasilisha barua za kujiuzulu kwa wakubwa wao.
“Ninadaiwa Sh15,000 na serikali hata baada ya kupata mshahara. Hii inamaanisha nitadaiwa Sh30,000 mwezi ujao na kiwango hicho kitaongezeka kila mwezi nikiendelea kufanya kazi katika huduma ya polisi,”afisa mmoja aliambia Taifa Leo.
Afisa huyo ambaye tayari amejiuzulu alisema alikuwa amechukua mkopo kwa sababu alikuwa na mshahara wa kutosha kulipa kila mwezi.
Makosa sana
“Ni makosa kupunguza mshahara mara moja bila kutupea notisi. Huu ni unyanyasaji,” alisema afisa huyo.
Alisema alilazimika kukopa pesa kufanikisha kujiuzulu kwake kwa sababu anahitajika kulipa serikali mshahara wa mwezi mmoja na kutoa notisi ya saa ishirini na nne au kutoa notisi ya kuacha kazi ya miezi mitatu jambo ambalo wengi hawataki.
Ikiwa mtu hataki kulipa mshahara wa mwezi mmoja na kutoa notisi anapaswa kutoa notisi ya miezi mitatu jambo ambalo maafisa hao hawataki.
Ni maafisa waliohudumu kwa miaka 12 wanaostahili kupata marupurupu wakijiuzulu. Maafisa wa polisi wa cheo cha konstebo walio na digrii wamekuwa wakipata mshahara wa chini wa Sh36,000 na marupurupu ya Sh11,000.
Baada ya NPSC kupunguza mishahara yao kufuatia agizo la Afisa Mkuu Mtendaji, Joseph Onyango, maafisa hao sasa watakuwa wakipata mshahara wa Sh18,000 na marupurupu ya Sh9,000, sawa na wale ambao hawana digrii.
Jumapili Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU), Francis Atwoli alisema hatua ya NPSC ni kinyume na azimio la Shirika la Leba ulimwengun (ILO) linalosema kuwa mfanyakazi hapaswi kupunguziwa mshahara wake.