MAPISHI: Jinsi ya kuandaa vipapatio vya kuku vyenye asali
Na MARGARET MAINA
Muda wa kuandaa: Dakika 20
Muda wa kupika: Dakika 40
Walaji: 4
Vinavyohitajika
- Kilo 1 ya vipapatio vya kuku
- Vitunguu saumu 4, menya kisha saga
- Vijiko 3 vya asali
- Kijiko 1 cha soy sauce
- Kijiko 1 cha pilipili ya unga
- Mafuta ya kupikia
- Juisi ya limau
- Chumvi
Maelekezo
Anza kwa kuviandaa vipapatio vya kuku. Vioshe vizuri kisha weka kwenye chombo kilicho safi.
Ongeza juisi ya limau, weka chumvi nusu kijiko na pilipili.
Koroga vizuri kwa mikono hadi zichanganyike vizuri. Hifadhi kwenye jokofu kwa muda wa saa mbili ili viungo vichanganyike na nyama ya kuku vizuri.
Weka kikaangio chenye mafuta mekoni. Mafuta yakipata moto, weka kuku huku ukigeuza mara kwa mara.
Acha nyama ya kuku iive vizuri kisha toa na uhifadhi pembeni au kando.
Kwenye kikaangio tofauti, mimina mafuta ya kupikia kisha bandika kwenye meko yenye moto wa wastani.
Mafuta yakipata moto, weka kitunguu saumu. Koroga na acha kiive hadi kianze kubadilika rangi; kuwa makini uhakikishe hakiungui.
Weka asali, soy sauce, na pilipili. Koroga vizuri. Acha vichemke na kuchanganyika kwa muda wa dakika moja.
Weka vipapatio vya kuku, koroga vizuri zaidi. Ongeza moto ili asali na soy sauce vitoe povu kiasi, na kutoa hali au dalili ya kama kuungua na kunata.
Epua, pakua na ufurahie.