• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Maraga awashauri magavana na wabunge kujadiliana kwanza

Maraga awashauri magavana na wabunge kujadiliana kwanza

MAUREEN KAKAH na CHARLES WASONGA

MAHAKAMA ya Juu Jumanne ilizitaka pande husika katika kesi ambapo magavana wanataka ufasiri na ushauri wake kuhusu mswada wa ugavi wa mapato kusuluhisha mvutano kuhusu suala hilo kupitia mazungumzo.

Jaja Mkuu David Maraga alisema majaji wote wa mahakama hiyo wameamua kwa kauli moja kwamba, kesi iliyowasilishwa mbele yao inahusu suala la utengenezaji sheria ambalo linapasa kusuluhishwa na wanachama wa bunge la kitaifa na wenzao wa seneti.

Alisema Mahakama ya Juu haiko tayari kuingilia mvutano kati ya mabunge hayo mawili kuhusu mswada huo ndiposa akazipa pande husika hadi Jumatano juma lijalo kuelewana kwa njia ya mazungumzo.

“Naelewa kwamba shughuli katika serikali za kaunti zimekwama. Tumekutana leo asubuhi kama majaji wa Mahakama ya Juu, tunahisi kwamba hatuwezi kuingilia suala kama hili ambalo linahusu mchakato wa utengenezaji sheria,” akasema Bw Maraga.

Akaongeza: “Ni wajibu wa mabunge haya mawili kuendeleza wajibu huu kivyao bila kuingiliwa.Majaji wanauliza mbona bunge linatuingiza katika suala ambalo wanaweza kusuluhisha?”

Mahakama hiyo ilielezwa kwamba, Bunge la Kitaifa na Seneti tayari kila moja limechapisha mswada wa ugavi wa mapato na kuanza haraka ya kutafuta maoni ya umma kuihusu.

Mahakama hiyo pia iliambiwa kuwa, huenda pande husika zikapata mwelekeo kuhusu suala hilo mnamo Alhamisi (kesho) ikizingatiwa kuwa kila bunge limewasilisha mswada wake kwa mjadala bungeni.

Mswada wa Ugavi wa Mapato ulitayarishwa na Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Bajeti inayoongozwa na Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichungwa. Mswada huo unapendekeza kwamba serikali za kaunti zitengewe Sh316 bilioni katika mwaka huu wa kifedha wa 2019/2016.

Na kwa upande wake, Mswada aina hiyo ulioandaliwa na Kamati ya Seneti kuhusu Fedha na Bajeti unapendekeza kuwa serikali za kaunti zitengewe Sh335 bilioni, kiasi sawa na kilichopendekezwa na Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA).

Juni, mabunge haya mawili yalikosa kuelewana kuhusu suala hilo hata baada ya kamati ya upatanisho kubuniwa. Hali hiyo ilipelekea Bajeti ya Kitaifa kusomwa bungeni mnamo Juni 13 kabla ya mswada wa ugavi wa mapato kupitishwa, kama inavyohitajika kisheria.

Hata hivyo, Bunge la Kitaifa limewakashifu magavana kwa kupotosha mahakama na umma kwa ujumla kwamba, kuna mzozo kuhusu suala hilo. Lakini Seneti iliambia mahakama kwamba, licha ya kuwepo kwa mazungumzo ya muda mrefu kuhusu suala hilo, muafaka haujapatikana.

Kulingana na Seneti, endapo makubaliano hayatapatikana kuhusu suala hilo, mahakakama inapasa kutoa uamuzi wake kulihusu.

Lakini Jaji Maraga akajibu kwa kusema: “Tunataka kuzipa pande husika nafasi ya kushughulikia kivyao. Na kuna imani kwamba mtapata suluhisho ambalo litafaa kila mtu.

You can share this post!

Dhamana ya Sh30m kwa Rotich na Thugge au Sh100m pesa taslimu

Sonko aiga Rais, ateua msimamizi wa shughuli za wizara zote

adminleo