Habari

Takwa la chapati kupikwa mazishini mwa mtoto aliyejinyonga latimizwa

March 19th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na JOHN NJOROGE

FAMILIA ya mwanafunzi wa darasa la sita wa shule moja eneo la Molo aliyeacha ujumbe wenzake wapikiwe chapati kisha akajinyonga, Jumatatu ilitimiza takwa lake kwenye mazishi yake.

Mtoto huyo Joseph Nehemiah Muluka, 15, alizikwa katika boma la baba yake katika kijiji cha Michatha Kaunti Ndogo ya Molo. Mvulana huyo aliyekuwa akisomea shule ya msingi ya Sulgwita iliyoko Turi alijitia kitanzi wiki baada ya kudaiwa kuiba Sh100 za dada yake.

Wingu la simanzi lilitanda katika kijiji hicho alipokuwa akizikwa japo kulikuwa na mlo wa chapati alivyotaka.

Kwenye ujumbe alioacha ambao ulipatikana karibu na mwili wake, mvulana huyo alieleza jinsi alivyowapenda ndugu na dada zake na akaomba wazazi wake kuwapikia chapati kwa wingi wakati wa mazishi yake.

Jumatatu, baba yake Bw Daniel Majimbo alifichua kuwa alitimiza ombi hilo na kuwapikia dada na ndugu wa marehemu chapati kwa wingi.

Wakazi waliopigwa na butwaa watazama chumba ambamo mwanafunzi huyo alijitia kitanzi Machi 14, 2018 katika kijiji cha Michatha, Molo, kaunti ya Nakuru. Picha/ John Njoroge.

“Tuliwapikia chapati marafiki wote na waombolezaji waliofika kwenye mazishi,” alisema Bw Majimbo.  Alisema marafiki akiwemo aliyekuwa diwani wa wadi ya Turi, walitoa unga wa ngano.

Chifu wa eneo hilo Bw Jackson Njoroge ambaye pia alihudhuria mazishi hayo alisema visa vya vijana kujitia kitanzi vimeongezeka mno katika kijiji hicho.

Aliitaka serikali ya kaunti kufunga vyumba vya kucheza kamari na burudani ambazo zinawavutia vijana kuwa na tabia mbaya.
Miongoni mwa waombolezaji walikuwa marafiki wa marehemu ambao walifurahia chapati alivyotaka.

Wazazi wake, marafiki na walimu walimtaja kama mvulana aliyekuwa mpole na mnyenyekevu ambaye aliwaheshimu pamoja na ndugu na dada zake.