• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Wakenya hutumia WhatsApp, Facebook sana usiku – Utafiti

Wakenya hutumia WhatsApp, Facebook sana usiku – Utafiti

Na PETER MBURU

WAKENYA wengi hutumia kati ya saa moja na tatu kila siku katika mitandao ya kijamii, kulingana na utafiti ambao umefanywa.

Utafiti huo uliofanywa na chuo kikuu cha USIU na ubalozi wa Marekani nchini ulibaini kuwa Wakenya wengi wa kati ya miaka 21-25 hutumia kati ya saa mbili na tatu mitandaoni, huku wale wa kati ya miaka 26-35 wakitumia takriban saa moja kwa siku kwenye WhatsApp, Facebook na Twitter.

Wakenya wa zaidi ya miaka 46 walibainika kuwa wanaotumia muda mchache zaidi kuwa mitandaoni, utafiti huo ukaongeza, ukisema wengi wa watumizi wa mitandao huitumia nyakati za usiku, hasa wanapofika nyumbani kutoka kazini.

Saa nyingine ambayo watu wengi hutumia mitandao ni jioni, kisha asubuhi na alasiri mtawalia, utafiti huo ukasema.

Utafiti wenyewe ulikuwa ukitaka kubaini jinsi Wakenya wanatumia mitandao ya kijamii, ambapo watu 3,269 walihojiwa, wote wa kati ya miaka 14 na 55.

Ni utafiti ambao ulifanywa wakati kumekuwa na tetesi kuwa muda mwingi ambao Wakenya wanatumia katika mitandao ya kijamii unaishi kuathiri shughuli za kikazi, na uhusiano wa kibinafsi.

Kitu kingine kilichobainika katika utafiti huo ni kuwa wanaume wanatumia mitandao ya kijamii kuliko wanawake, wengi wao wakitumia Yahoo na Twitter kwa wingi zaidi.

Wanawake nao hutumia kwa wingi mitandao ya Snapchat na Twitter kwa wingi zaidi, utafiti ukasema.

Baadhi ya sababu kuu zilizobainika kuwa zinazowapeleka Wakenya mitandaoni ni kupata habari, burudani na kujihusisha na marafiki.

Mitandao inayoongoza kwa umaarufu nchini ni Whatsapp kwa asilimia 88.6, kisha Facebook kwa asilimia 88.5, wengi wa wanaoitumia wakiwa wa kati ya miaka 25 na 35.

“Wakenya wengi sasa wanatumiua simu kuingia Intaneti, kinyume na mbeleni ambapo ilikuwa kwenda kwa saibakafe. Hata hivyo, baadhi ya Wakenya wa mashambani na wanaoishi maeneo ya kimaskini mijini bado wanatumia saibakafe,” ripoti hiyo ikasema.

Naibu Chansela wa USIU Paul Zeleza alisema mitandao ya kijamii ina uwezo wa kuajiri vijana wengi kwa sasa, alipozungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo.

You can share this post!

Hisia mseto serikalini baada ya Ukur Yattani kujaza nafasi...

Mwanamume ashtaki korti kwa kumfanyia upasuaji wa...

adminleo