• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Kauli za Boris Johnson kuhusu Afrika zaanika hisia zake za ubaguzi

Kauli za Boris Johnson kuhusu Afrika zaanika hisia zake za ubaguzi

Na MASHIRIKA

KAULI za zamani za Waziri Mkuu mpya wa Uingereza Boris Johnson zimezua hofu kuwa huenda uhusiano wa nchi hiyo na mataifa ya Afrika ukadorora.

Bw Johnson alichukua hatamu za uongozi Jumatano dakika chache baada ya mtangulizi wake Theresa May kuwasilisha rasmi barua ya kujiuzulu kwa Malkia Elizabeth.

Kwa mujibu wa Katiba, Bi May alimpendekeza Bw Johnson kwa Malkia kuwa kiongozi anayefaa kuongoza serikali ya Uingereza.

Baadaye, Boris alitakiwa kupiga busu mkono wa Malikia na kisha kutangaza baraza lake la mawaziri.

Johnson alichaguliwa Jumanne kuwa kiongozi wa chama cha Conservative Party, wadhifa ulioachwa na May aliyetangaza kujiuzulu mwezi uliopita.

Hata hivyo, ulimwengu unasubiri kwa hamu na ghamu kuona jinsi Bw Johnson atahusiana na mataifa ya Afrika baada ya kauli zake za hapo awali kuonekana kusheheni matamshi ya ubaguzi wa rangi.

Mbali na kutoa kauli za kudunisha Afrika, Johnson pia amewahi kutoa matamshi ya kudhalilisha wanawake.

Mnamo 2018, Bw Johnson aliandika katika gazeti la Teregraph akisema kuwa, wanawake wa Kiislamu wanaovalia hijabu wanafanana na masanduku ya kubebea barua.

Baraza Kuu la Waislamu la Uingereza lilimshutumu kwa kutoa kauli hiyo na chama cha Conservative party kilimchunguza kuhusiana na matamshi hayo.

Mnamo 2017, Bw Johnson aliandika kuwa nchi ya Libya huenda ikawa na maendeleo makubwa kama Dubai endapo ‘maiti’ itatolewa.

“Libya inaweza kugeuka kuwa Dubai lakini wanachohitaji ni kuondoa maiti yote,” akasema Johnson.

Baadaye, alikataa kuomba msamaha kwa matamshi hayo.

Alipokuwa waziri wa mashauri ya kigeni wa Uingereza mnamo Oktoba 2016, alirejelea bara la Afrika kama ‘nchi hiyo’.

Mnamo Aprili 2016, Bw Johnson alisema kuwa aliyekuwa rais wa Amerika Barack Obama alichukia Uingereza kwa sababu alikuwa Mkenya.

Mnamo Julai 2013: alidai kuwa wanawake wanaenda katika vyuo vikuu kutafuta wanaume wa kuwaoa.

Makundi ya kutetea haki za wanawake yalimshutumu Johnson kutokana na matamshi hayo na kumtaka kuomba radhi. Mnamo Januari 2002, Bw Johnson alisema Malkia Elizabeth anapenda nchi za Afrika kwa sababu zina watoto wa kumshangilia huku wakipeperusha bendera ya Uingereza.

‘‘Ikiwa Afrika inahitaji kujiinua kiuchumi basi haina budi kufuata nyayo za wakoloni wao wa zamani ambao ni Uingereza,” akaandika Bw Johnson katika makala yake iliyochapishwa katika gazeti la The Sun.

You can share this post!

Kenya kuuza mafuta ng’ambo chini ya mpango wa majaribio

AKILIMALI: Kiwanda cha maziwa chapiga jeki uchumi wa wakazi...

adminleo