• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Magoha akosoa vyuo vikuu kwa kupinga azma ya kuviunganisha

Magoha akosoa vyuo vikuu kwa kupinga azma ya kuviunganisha

NA OUMA WANZALA

WAZIRI wa Elimu Prof George Magoha Jumatatu aliwakejeli Manaibu Chansela wa vyuo vikuu vya umma ambao wanapinga mpango wa kuviunganisha huku vikizongwa na matatizo ya kifedha.

Prof Magoha akihutubia mkutano wa wahariri jijini Nairobi, alisisitiza kwamba cha muhimu ni ubora wa elimu unaotolewa na vyuo vikuu wala si wingi wa vyuo hivyo.

“Niliagizwa na Rais Uhuru Kenyatta baada ya kuteuliwa kwamba kusiwe na vyuo vikuu vingine vipya. Lazima tulainishe sekta ya elimu kwenye vyuo vyetu vikuu,” akasema Prof Magoha.

Juni, Prof Magoha aliwaamrisha wakuu hao wa vyuo kuibuka na mbinu ya kuviunganisha lakini kwenye mapendekezo waliyowasilisha kwake walikataa wakisema si jambo lenye umuhimu kwa sasa.

Manaibu Chansela 31 wa vyuo vikuu vya umma badala yake walipendekeza vyuo vingine 100 vianzishwe kwa kuwa idadi ya wanafunzi wanaojiunga navyo itakuwa imetinga milioni moja kufikia mwaka wa 2030.

Hata hivyo, Prof Magoha alishikilia kwamba Katiba inapendekeza kila kaunti iwe na chuo kikuu lakini haijabainisha ni lini hasa hilo linafaa kuafikiwa akiongeza kwamba linaweza kuwa hata baada ya miaka 100.

Waziri huyo msomi pia hakusaza vyuo ambavyo vinafundisha kozi nyingi zinazofanana kwa njia moja au nyingine ili kupata faida ya kifedha, akiwaamrisha wafutilie mbali kozi hizo.

Aidha alitaka Tume ya elimu ya vyuo vikuu (CUE) kuharakisha utayarishaji wa ripoti kuhusu kuunganishwa kwa vyuo vikuu na kuwapa makataa ya hadi kesho kuiwasilisha kwa afisi yake.

You can share this post!

Madiwani ngome ya Ruto waunga mkono ‘Punguza Mizigo’

Mganga wa TZ anayedai kufufua maiti akamatwa Taveta

adminleo