• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Wapigakura Misri watishia kususia uchaguzi

Wapigakura Misri watishia kususia uchaguzi

Na MASHIRIKA

BAADHI ya wapigakura nchini wametishia kususia uchaguzi utakaofanyika wiki ijayo huku aliyekuwa msemaji wa kiongozi wa Uganda Rais Yoweri Museveni akiteuliwa kuongoza ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi wa Muungano wa Masoko Mashariki na Kusini mwa Afrika (Comesa) nchini Misri.

Uchaguzi nchini Misri ni kati ya Machi 26 na 28.

Kiongozi wa sasa, Rais Abdel-Fattah al-Sisi anapigiwa upatu kushinda uchaguzi huo baada ya kukamata na kufunga wapinzani wake. Wapinzani wengine wa Rais Sisi walitishiwa na kulazimika kujiondoa kutoka kinyang’anyiro hicho.

Rais Sisi anakabiliana na Moussa Mostafa Moussa, ambaye ni mshirika wake wa muda mrefu.

Wadadisi wa kisiasa wanasema Moussa asiye na ushawishi alifadhiliwa na Rais Sisi kuwania urais ili kiongozi huyo asionekane kuwa mwaniaji wa pekee.

Wengi wa Wamisri walioshiriki katika maandamano ya kumng’oa mamlakani Hosni Mubarak, kiongozi wa muda mrefu aliyeongoza nchi hiyo kwa karibu miaka 30, mnamo 2012, waliapa kuwa hawatashiriki katika uchaguzi huo.

Sisi akiwa waziri wa Ulinzi aliongoza maandamano ya kumng’oa mamlakani rais wa kiislamu Mohamed Morsi mnamo Julai 2013. Kulingana na taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Comesa Mwangi Gakunga, muungano huo uliamua kupeka ujumbe wa waangalizi baada ya kupokea mwaliko kutoka kwa Tume ya Uchaguzi ya Misri (NEC).

Muungano wa Comesa unajumuisha Burundi, Comoros, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Djibouti, Misri, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Libya, Madagascar, Malawi, Mauritius, Rwanda, Seychelles, Sudan, Swaziland, Uganda, Zambia na Zimbabwe.

“Bi Hope Kivengere ataongoza ujumbe wa waangalizi wa Comesa,” ikasema taarifa hiyo. Ujumbe wa Comesa utakutana na vyama vya kisiasa, maafisa wa tume ya NEC, mashirika ya kijamii na washikadau wengine na kutoa ripoti yake ya awali kabla ya uchaguzi.

Ripoti ya kina ya Comesa itakabidhiwa kwa tume ya NEC na serikali ya Misri siku 90 baada ya uchaguzi.

Wamisri wanaoishi ughaibuni walianza kupiga kura Ijumaa iliyopita. Runinga ya serikali ya Misri ilionyesha maelfu ya raia wake wakipiga kura katika balozi za Kuwait, Saudi Arabia na Miliki za Uarabuni (UAE).

“Hakuna haja ya uchaguzi, Rais Sisi tayari ameshinda kwani mpinzani wake hajakuwa akifanya kampeni, anaigiza,” akasema Mmisri aliyetaka jina lake libanwe.

You can share this post!

TAHARIRI: Muafaka usiwe kifo cha upinzani

Walanguzi wote wa dawa za kulevya wanyongwe – Trump

adminleo