• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 6:55 AM
Wanaswa wakisafirisha nyama ya nyati hadi Burma, Nairobi

Wanaswa wakisafirisha nyama ya nyati hadi Burma, Nairobi

Na CHARLES WASONGA

MAAFISA wa Shirika la Wanyamapori Nchini (KWS) Jumanne walinasa washukiwa watatu akiwemo mfanyabiashara mmoja wa Naivasha wakisafirisha kilo 200 za nyama ya nyati ikisafirishwa hadi soko la nyama jijini Nairobi, Burma.

Watu hao walikamatwa katika katika eneo la Marula farm kando ya barabara ya Nakuru-Nairobi wakisafirisha nyama hiyo kw gari moja la kibinafsi.

Washukiwa hao walikamatwa siku chache baada ya mafisa hao kuwakamata washukiwa wawili katika barabara hiyo wakiwa na pembe ya ndovu ya uzani wa kilo 14.

Katika kisa cha Jumanne, watatu hao walikamatwa wakipakia nyama ndani ya gari hilo baada ya maafisa hao wa KWS kupashwa habari na walinzi waliokuwa wakifanyaka kazi katika shamba hilo.

Kulingana na mkurugenzi wa KWS anayesimamia eneo la Centrali Rift Aggrey Maumo, visa vya watu kuuza nyama ya wanyama wa porini vimekithiri katika eneo hilo.

“Habari za kijasusi tulizopokea zinaonyesha kuwa kiasi kikubwa cha nyama ya wanyamapori ambayo hupelekwa kuuzwa katika soko la Burma, Nairobi hutoka Naivasha na Gilgil. Na tutahakikisha kuwa tunakomesha uhalifu huu,” akasema.

Bw Maumo alisema wanyama wengi huwindwa na wafanyabiashara hao walaghai kutoka maeneo ya Hells Gate, mbuga ya kitaifa ya Mt Longonot na hifadhi za wanyama zilizo karibu.

“Kuna wanyama wengi ambao hutoroka kutoka kwa mbunga na ranchi za mbali na ndio huuawa na wafanyabiashara hao haramu ili wauze nyama kwa wateja wasio na ufahamu,” akasema.

Afisa huyo alisema kuwa watu hao wamekuwa wakiwalenga nyati na pundamilia kwa sababu nyama yao inafanana kwa karibu na nyama ya ng’ombe.

Bw Maumo aliongeza kuwa KWS inashirikiana na jamii za eneo hili kupambana na wahusika katika uhalifu huo akiongeza kuwa asasi hiyo imebuni kikosi maalum kukabilina walaghai hao.

Itakumbukwa kwamba mnamo Januari mwaka huu, wafanyabiashara 15 walikamatwa katika Soko la Burma wakiwa na kilo 800 ya nyama ya pundamilia.

Maafisa wa usalama ambao walishirikiana na wale wa KWS walisema nyama hiyo ilikuwa ikiuziwa wateja kama nyama ya ng’ombe.

Kulingana na maafisa wa KWS, walikuwa wakiwafuata wafanyabiashara hao baada ya wao kuonekana wakitosha pundamilia katika Portlanda Farm, Athi River, kaunti ya Machakos.

Uwindaji haramu umekithiri katika miji inayopakana na Nairobi kutokana na uwepo wa soko kubwa la nyama katika eneo la Burma.

You can share this post!

Olunga amega pasi mbili zilizozalisha magoli

Kesi ya Karua dhidi ya Gavana Kamotho yagonga mwamba

adminleo